0712461976
TIMU ya taifa ya Tanzania, Taifa
stars chini ya kocha mkuu, Mholanzi, Mart Nooij inatarajia kucheza mechi
ya kwanza ya raundi ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za
Afrika 2015 nchini Morocco dhidi ya Zimbabwe (Mighty Warriors) jumapili
mei 18 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Taifa Stars wataingia katika mechi hii baada ya kushindwa kupata ushindi katika mechi mbili za kirafiki.
Aprili 26 mwaka huu walicheza na
Burundi ndani ya uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam na kufungwa mabao
3-0. Lakiki kikosi cha stars kilisheheni wachezaji kutoka katika mpango
wa maboresho ya Taifa Stars.
Mei 4 mwaka huu kwenye uwanja wa
Sokoine jijini Mbeya, Stars ilicheza mechi ya pili ya kirafiki dhidi ya
Malawi na kulazimisha suluhu pacha ya bila kufungana.
Mechi dhidi ya Burundi, tatizo
kubwa kwa Taifa stars lililkuwa kukosa uzoefu kwa wachezaji wapya.
Vijana waliotokea katika mpango wa maboresho walikuwa waoga,
hawakujiamini hata kidogo na hawakuwa na nidhamu ya mchezo.
Burundi walikuwa na kazi ndogo ya
kuwafunga Stars, huku wachezaji wazoefu na mechi za kimataifa kama Deo
Munish, Saimon Msuva, Frank Domayo, Ramadhan Singano `Messi` wakijaribu
kuokoa jahazi bila mafanikio.
Akina Omari Nyenye kutoka
maboresho ya Stars walichezea nafasi za wazi na kuwaruhusu Burundi
kuwaliza watanzania siku muhimu ya maadhimisho ya miaka 50 ya muungano
wa Tanganyika na Zanzibar.
Hata hivyo jana zilienea taarifa
kuwa wachezaji watano wa Taifa stars akiwemo Nyenye, wametemwa. Wengine
wanaosemekana kuachwa na kocha Nooij ni mshambuliaji Hussein Javu, beki
Hassan Mwasapili, wengine ni Ammanuel Namwando na Michael Pius.
Bila shaka sababu ya kuwaacha wachezaji hawa ni ya kimpira na mwalimu Nooij ndiye mtaalam anayefahamu vizuri kwanini amewatema.
Katika mchezo dhidi ya Malawi,
Taifa stars iliwatumia wachezaji waliozoeleka na wenye uzoefu kama
Deogratius Munish `Dida`, Erasto Nyoni, Oscar Joshua, Nadir Haroub
`Canavaro`, Agrey Morris, Frank Domayo, Jonas Mkude, Saimon Msuva,
Ramadhan Singano, Harun Chanongo, Amri Kiemba, John Bocco na wengineo.
Lengo la Nooij lilikuwa ni
kutafuta wachezaji wa kuwatumia katika michezo ya kimataifa ya
mashindano kuanzia wa jumapili dhidi ya Zimbabwe.
Katika mechi hii, Stars ilicheza
vizuri hasa safu ya ulinzi chini ya maaskari wawili wa kati, Nadir
Haroub ` Canavaro` na Agrey Morris.
Wanaume hawa kwa kushirikiana na
mabeki wao wa pembeni, Erasto Nyoni na Oscar Joshua, waliifanya ngome ya
Stars kuwa ngumu kupitika.
Hata hivyo bado kulikuwa na makosa ya kimchezo ambayo mwalimu atakuwa ameyafanyia kazi.
Pia katika safu ya Kiungo vijana
walicheza vizuri na kupeleka mipira mingi mbele, lakini tatizo kubwa
lilibaki katika safu ya ushambuliaji.
John Raphael Bocco na wenzake
walikosa nafasi nyingi za kufunga na hata baada ya mechi Kocha Nooij
aliwalaumu washambuliaji wake kwa kukosa umakini, na akaahidi kufanyia
kazi tatizo hilo.

Zimbabwe walikuwa hatari mno na
kuidhihirishia dunia kuwa mpira umeanza kuhamia katika ardhi yao.
Zimbabwe wanacheza kwa kujituma na kwa asilimia kubwa wachezaji wao
wanajitolea kwa ajili ya timu.
Moja kati ya matatizo ya wachezaji wa Tanzania ni kushindwa kujitolea kwa moyo wote.
Mpira una kanuni kuwa kama timu
yako imezidiwa, na mchezaji unafahamu kuwa kwa jitihada zako binafsi
unaweza kuokoa jahazi, basi cheza kwa faida ya timu na jitolea kwa nguvu
zote.
Lakini kwa wachezaji wetu wanaonekana kucheza kawaida tu bila kutambua wapo wakati gani na timu inahitaji nini.
Mechi ya jumapili ni ngumu kwa Taifa stars kutokana na maendeleo makubwa waliyopata Zimbabwe.
Wana watu kule mbele kama
Knowledge Musoma, Kingston Nkhatha. Hawa jamaa kama watakuwepo jumapili,
ni shughuli pevu kwa mabeki wa Stars.
Hata hivyo masikitiko makubwa kwa
Taifa stars ni kuwakosa wachezaji wawili wanaocheza soka la kulipwa
katika klabu ya TP Mazembe ya DRC, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.
Kwa vyovyote vile, wachezaji hawa
walikuwa muhimu katika mchezo wa jumapili kutokana na uzoefu wao na
kiwango walichonacho kwa sasa, lakini kwa kuwa yameshatokea haya, basi
ni kuwaangalia waliopo sasa.
Ili Taifa Stars washinde mechi ya jumapili, haya ni baadhi ya mambo machache kati ya mengi wanayotakiwa kufanya;
Mosi; watulize akili kujiandaa na
mchezo huo. Kwa muda sasa wamekuwepo eneo tulivu la Tukuyu kwa
maandalizi yao. Wamebakiza siku chache kufikia jumapili, hivyo lazima
akili yao ielekee katika mechi hii na kuachana na mambo mengine.
Pili; watambue kuwa wapo uwanja
wa nyumbani. Siku hizi mpira umebadilika sana, hata ukiwa nyumbani
unachezea kichapo. Lakini kuna faida ya kucheza nyumbani. Unakuwa na
faida ya uwanja wako, mashabiki wako, hivyo unakuwa na sapoti ya kila
kitu hata mazingira pia.
Hata ulaya, timu nyingi huwa zinamaliza biashara nyumbani. Kwahiyo stars watambue kuwa watakuwa nyumbani, lazima wacheze kwa malengo ya kutafuta ushindi.
Hata ulaya, timu nyingi huwa zinamaliza biashara nyumbani. Kwahiyo stars watambue kuwa watakuwa nyumbani, lazima wacheze kwa malengo ya kutafuta ushindi.
Kuwafunga Zimbabwe zaidi ya mabao
matatu itakuwa faida kubwa kwasababu kuwafunga Harare itakuwa ngumu
sana. Vijana watumie vizuri nafasi ya nyumbani.
Tatu; wasicheze na majukwaa.
Taifa stars siku za karibuni imekuwa na hali mbaya kwa mashabiki. Mara
kadhaa huwa wanaizomea inapocheza. Hivyo wachezaji wasijali kama
itatokea hali hii, waingie kufanya kazi yao na kutafuta kushangiliwa kwa
soka zuri. Kama watafunga hakuna atakayewazomea. Na kwakuwa wanajua
watanzania wanawazomea, basi watafute namna ya kuwafanya wawashangilie.
Uzelendo kwa mashabiki wa kibongo bado sana, hivyo vijana wawalazimishe kuwapa sapoiti kwa kucheza vizuri.
Nne;Wapunguze makosa sehemu ya
kiungo na ulinzi. Safu ya Canavaro, Morris ilikuwa imara dhidi ya
Malawi. Hawakupitisha mipira ya hatari kirahisi, lakini kulikuwa na
makosa madogo madogo ambayo kama Malawi wangekuwa na watu makini basi
wangeifunga Stars. Kikubwa watambue kuwa kuna Musoma ambaye hafanyi
makosa anapota nafasi.
Viungo wajipange kuziba eneo la
kati vizuri ili kuwasaidia mabeki kucheza kwa kutulia. Kama Zimbabwe
watashambulia kutokea pembeni, basi akina Oscar na Nyoni wajiandae
kukabiliana kwa nguvu ili kuwarahisishia kazi mabeki wa kati.
Tano; Safu ya ushambuliaji ya Taifa stars itatakiwa kutumia
vizuri nafasi watakazopata. Kama watazichezea nafasi kama kule Mbeya
dhidi ya Malawi, basi kusonga mbele itakuwa ndoto. Bocco na wenzake
lazima watambue kuwa wapo nyumbani na timu inahitaji magoli ili kujiweka
nafasi nzuri.
Timu itatakiwa kushambulia kwa
kasi na kwa muda wote. Lakini kujilinda itakuwa muhimu pia. Stars waje
kwa mtazamo wa kumiliki mpira na kucheza pasi murua,lakini kulinda eneo
la iyakuwa muhimu zaidi na kushambulia kwa kasi kubwa.
Sita; mashabiki wanatakiwa
kujitokeza na kuwashangilia wachezaji wa Taifa stars. Katika mpira
mashabiki ni muhimu. Ni sawa na mchezaji wa 12. Hivyo watanzania kwa
moyo mmoja wajitokezea na kuwashangilia stars. Wachezaji wanajiona wana
thamani kubwa wanaposikia amsha amsha za mashabiki uwanjani.
Zipo sababu nyingi za kuifanya
Taifa stars ipate matokeo jumapili ya mei 18, lakini hizo ni chache
miongoni mwa sababu nyingi. Mtandao huu utaendelea kukupatia sababu
nyingine kadri tunavyokaribia siku ya mechi.
Taifa Stars watanzania tupo nyuma yenu. Fanyeni kazi yenu kwa faida ya Taifa.
Taifa Stars ambayo ilikuwa kambini mkoani Mbeya itarejea Dar es Salaam kesho (Mei 14 mwaka huu) kujiandaa kwa mechi hiyo.
0 comments:
Post a Comment