Searching...
Tuesday, April 15, 2014

MAMIA WAJITOKEZA UWANJA WA NDEGE KUWALAKI WAFALME WAPYA WA SOKA YA TANZANIA, AZAM FC

MAMIA ya wapenzi na mashabiki wamejitokeza jioni ya leo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam kuipokea timu ya Azam FC ikitokea Mbeya ambako jana iliwafunga wenyeji, Mbeya City mabao 2-1 na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Kikosi cha Azam kiliwasili kwa ndege majira ya Saa 12:00 jioni na kulakiwa na mamia ya wapenzi kabla ya kupanda basi lao la kisasa kuelekea makao yao makuu, Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam. 
Ilikuwa hoi hoi, nderemo na vifijo katika mapokezi ya timu hiyo ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake katika mapokezi yake baada ya mabingwa hao wapya wa Bara kutua JNIA.
Mashabiki wakiilaki Azam FC jioni ya leo Uwanja wa Ndege Dar es Salaam

Azam ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jana, baada ya kuifunga Mbeya City mabao 2-1 Uwanja wa Sokoine mjini hapa, huku waliokuwa wapinzani wao katika mbio za taji hilo, Yanga SC wakishinda 2-1 dhidi ya JKT Oljoro mjini Arusha jana pia. 
Azam imefikisha pointi 59 ikiwa na mchezo mmoja mkononi ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote baada ya mechi za mwisho Aprili 19, mwaka huu. Yanga SC yenye pointi 55 sasa ikiifunga Simba SC Aprili wiki ijayo itafikisha 58.
Mabao ya Azam jana yalifungwa na Gaudence Mwaikimba na John Bocco, wakati la Mbeya City lilifungwa na Mwagane Yeya. 
Mashabiki wakiwa na mabango na mafano wa Kombe Uwanja wa ndege
Mashabiki wakicheza Uwanja wa ndege
Wachezaji wa Azam FC wakiwasili
Kulia ni Abubakar Mapwisa akiwasili na wachezaji
Kushoto Brian Umony na wachezaji wenzake

Azam walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 43, mfungaji Gaudence Mwakimba aliyemalizia pasi nzuri ya beki wa kulia Erasto Nyoni.
Baada ya bao hilo, Mbeya City walicharuka na kufanya mashambulizi mawili hatari langoni mwa Azam, lakini hawakuweza kupata bao hadi kipyenga cha kuhitimisha kipindi cha kwanza kinapulizwa.
Kipindi cha pili, Azam waliingia na mfumo wa kucheza kwa kujihami ili kulinda bao lao, mbele wakimuacha Mwaikimbe pekee na John Bocco akashuka katikati huku Salum Abubakar ‘Sure Boy’ akimsaidia Kipre Balou kukaba kiungo cha chini.
Mfumo huo ulikabirisha mashambulizi mengi langoni mwa Azam na haikuwa ajabu Mbeya City walipokomboa bao dakika ya 70 kupitia kwa Mwagane Yeya baada ya kuuwahi mpira uliopanguliwa na kipa Aishi Manula kufuatia shuti la Deus Kaseke.
Bao hilo kidogo liliwachanganya Azam FC na Mbeya City wakauteka mchezo kwa dakika kadhaa, kabla ya shambulizi la kushitukiza kuipa ushindi timu ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa dakika ya 86, baadaa ya John Bocco kukutana na mpira uliorudishwa.
Wachezaji wa Mbeya City walimzonga refa Nathan Lazaro wa Kilimanjaro baada ya bao hilo na kusababisha mchezo kusimama kwa zaidi ya dakika tatu.
Refa huyo alitoa kadi nyekundu kwa Mwagane Yeya baada ya vurugu hizo. Askari wa jeshi la Polisi walilazimika kufanya kazi ya ziada baada ya mechi kwa kuwadhibiti mashabiki wa Mbeya City waliotaka kufanya vurugu na pia kuusindikiza msafara wa Azam FC.
Pamoja na kuwa timu ya kwanza kuifunga Mbeya City kwenye Uwanja wake jana, Azam FC pia inakuwa timu ya kwanza nje ya Simba na Yanga kutwaa ubingwa wa Bara tangu mwaka 2000 Mtibwa Sugar ilipofanya hivyo
Azam inakuwa timu ya saba nje ya Simba SC kutwaa taji la Ligi Kuu, baada ya Cosmo mwaka 1967, Mseto mwaka 1975, Pan Africans mwaka 1982, Tukuyu Stars mwaka 1986, Coastal Union 1988 na Mtibwa Sugar mara mbili mfululizo 1999 na 2000.

0 comments:

WELCOME URARY95 SPORTS NEWS BLOG | ADVERTISE YOUR BUSINESS HERE AT A CHEAP PRICE MORE INFORMATION CONTACT US: 0654315901 | Email: urary95@yahoo.com | KARIBU URARY95 SPORTS NEWS BLOG | TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA GHARAMA NAFUU KWA MAELEZO ZAIDI WASILIANA NASI: 0654315901 | Barua Pepe: urary95@yahoo.com
 
Back to top!