Searching...
Tuesday, July 26, 2011

TANZANIA YAPIGIA DEBE KISWAHILI UN

TANZANIA imeitaka Idara ya Habari na Mawasiliano ya Umma ya Umoja wa Mataifa (UN) kuhakikisha kuwa inaongeza idadi ya waandishi katika Idhaa ya Radio ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa ili iweze kutekeleza kwa ukamilifu majukumu yake ya ukusanyaji, utoaji na usambazaji wa taarifa zinazohusu shughuli za umoja huo.

Tanzania imetoa mwito huo wakati wa Mkutano wa 33 wa Kamati ya Habari ya Umoja wa Mataifa, ambapo pamoja na mambo mengine Kamati hiyo iliyoanzishwa mwaka 1978 ikiwa na wajumbe 113 kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, walipokea na kujadili taarifa ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kuhusu utendaji wa Idara hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Ofisa Ubalozi Mwandamizi, Maura Mwingira alisema katika mkutano huo, Tanzania inafarijika na kuridhishwa na namna ambavyo Kiswahili kupitia Radio ya Kiswahili ya UN kimeendelea kuwa kiungo muhimu cha mawasiliano.

Alisema kimepata umaarufu na kuongeza idadi ya watumiaji wa taarifa za idhaa hiyo licha ya kwamba ina wafanyakazi wachache.

Taarifa ya Katibu Mkuu wa UN iliyowasilishwa kwa wajumbe na Katibu Mkuu Msaidizi anayeongoza Idara ya Habari, Akito Akasaka, imeonesha kuwa , katika eneo la Radio ya Umoja wa Mataifa, hutoa taarifa zake katika lugha sita rasmi.

Kiswahili na Kireno, zimekuwa na mafanikio makubwa ambayo pia yamehusisha ongezeko la watumiaji wa taarifa zake. Lugha rasmi za Umoja wa Mataifa ni, Kiingereza, Kifaransa, Kiarabu, Kirusi, Kichina na Kihispania.

Kwa upande wa Idhaa ya Kiswahili, Akasaka amesema, Redio hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 2006, idadi ya watumiaji wa taarifa za idhaa hiyo imepanda kutoka asilimia moja wakati wa kuanzishwa kwake hadi kufikia asilimia 21, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa Radio Maarifa FM iliyoko Tanzania.

0 comments:

WELCOME URARY95 SPORTS NEWS BLOG | ADVERTISE YOUR BUSINESS HERE AT A CHEAP PRICE MORE INFORMATION CONTACT US: 0654315901 | Email: urary95@yahoo.com | KARIBU URARY95 SPORTS NEWS BLOG | TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA GHARAMA NAFUU KWA MAELEZO ZAIDI WASILIANA NASI: 0654315901 | Barua Pepe: urary95@yahoo.com
 
Back to top!