Wapatanishi wa Kiafrika katika mgogoro wa urais huko Ivory Coast wameondoka mjini Abidjan mikono mitupu kufuatia kugonga mwamba mazungumzo kati yao na Laurent Gbagbo, anayeng'ang'ania madaraka nchini humo.
Gbagbo amesisitiza kuwa atapinga mwito wowote unaomtaka kukabidhi madaraka kwa mpinzani wake Alassane Ouattara, shakhsiya ambaye jamii ya kimataifa ikiwemo Tume Huru ya Uchaguzi ya Ivory Coast zimemtaja kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi Novemba huko Ivory Coast.
Gbagbo ameelezwa kuwa atakabiliwa na nguvu za kijeshi, iwapo atakataa kuondoka madarakani.
Raila Odinga Waziri Mkuu wa Kenya, Marais Boni Yayi wa Benin, Ernest Koroma wa Sierra Leone na Pedro Pires wa Cape Verde jana usiku waliondoka Abdijan Ivory Coast na leo wanaelekea Nigeria kumtaarifu Rais Goodluck Jonathan Mwenyekiti wa hivi sasa wa jumuiya ya Ecowas kuhusu mazungumzo yao na Gbagbo.
Wakati huo huo Alassane Ouattara, mgombea aliyeshinda katika uchaguzi wa Rais nchini Kodivaa amekataa sharti lililotolewa na Laurent Gbagbo anayeng'ang'ania madaraka la kutaka kuundwe tume maalumu ya kuchunguza matokeo ya uchaguzi huo.
Televisheni ya France 24 imemnukuu Ouattara akitoa msimamo huo baada ya kukutana na wajumbe wa Umoja wa Afrika walioongozwa na Raila Odinga, Waziri Mkuu wa Kenya.
Kwenye mazungumzo yake na ujumbe huo wa AU, Gbagbo alisema yuko tayari kuondoka madarakani kwa sharti la kuundwa tume maalumu ya kuchunguza upya kura za Rais.
Hata hivyo Outtara amemtaka Gbagbo aondoke madarakani bila ya masharti yoyote na aheshimu matokeo ya kura kama zilivyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Outtara ameongeza kuwa, zoezi la uchaguzi nchini Ivory Coast lilisimamiwa kikamilifu na Umoja wa Mataifa na mjumbe maalumu wa Ban Ki-moon Katibu Mkuu wa umoja huo na matokeo ya uchaguzi huo kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi yanaonyesha kuwa yeye ndiye aliyeshinda hivyo hakuna haja tena ya kupoteza wakati wa kuundwa tume mpya ya kufuatilia suala hilo.
Ameongeza kuwa, Gbagbo ambaye Mahakama ya Katiba ilimtangaza mshindi wa uchaguzi huo, ana nia ya kupoteza wakati ili apate muda wa kutosha wa kuingiza silaha na kuwapa wanamgambo wake ili wazidi kuua raia.


0 comments:
Post a Comment