Searching...
Wednesday, December 15, 2010

Ocampo azua hofu kubwa Kenya

Kiongozi wa mashtaka wa mahakama ya kimataifa ya Uhalifu ICC, Loius Moreno Ocampo, anatarajiwa kutangaza majina ya Wakenya kadhaa anaowatuhumu kuhusika katika machafuko yaliyofuatia uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 uliokumbwa na utata.
Wafuasi wa upinzani mjini wakiandamana mjini Kisumu. Jumatano, Januari, 16, 2008
Zaidi ya watu 1, 200 waliuwawa na zaidi ya nusu milioni kuachwa bila makazi.
Katika mkataba wa amani uliofuatiwa, ilikubaliwa wale waliopanga au kufadhili machafuko hayo watakabiliwa na mkono wa sheria nchini Kenya au katika mahakama ya ICC mjini Hague.
Baada ya Kenya kushindwa kubuni mahakama maalum ya kuwahukumu washukiwa hao mahakama ya ICC ilichukuwa jukumu hilo.
Mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama hiyo Luis Moreno Ocampo, analenga kesi mbili katika machafuko hayo ya baada ya uchaguzi.
Atataja majina ya washukiwa sita.
Kila mmoja atapewa ilani ya kumtaka afike mbele ya mahakama hiyo, lakini iwapo watakataa au kuvuruga uchunguzi dhidi yao, Bw Ocampo ataomba kutolewa kwa hati ya kukamatwa kwao.
Wanasiasa wenye ushawishi mkubwa wanatarajiwa kutajwa katika orodha hiyo ya watu sita.
Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na hofu kubwa miongoni mwa wanasiasa ambao kwa kawaida hupuuza mfumo wa sheria.
Wengi wa Wakenya wanahisi mashtaka haya ni muhimu ili kukomesha kasumba ya kutoheshimu sheria.
Loius Moreno Ocampo
Loius Moreno Ocampo
Kenya imekumbwa na msururu wa uchaguzi uliokumbwa na ghasia, lakini uchaguzi wa mwaka 2007 uliokumbwa na utata, nusura ulitumbukize taifa hilo katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Baada ya mgawanyiko wa kikabila, jamii ziligeukiana kwa kupigana huku baadhi ya watu wakitiwa hamasa au hata kulipwa pesa na wanasiasa walafi kutekeleza mauaji.
Maafisa wa polisi walitumia nguvu kupita kiasi na kuua watu holela.
Silaha ziliwekwa chini wakati aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, alipopatanisha pande mbili hasimu kati ya Rais Mwai Kibaki, na Waziri Mkuu, Raila Odinga.
Kama sehemu ya mkataba huo wa amani, walikubaliana kuhakikisha wale waliohusika katika machafuko hayo, wanashtakiwa nchini Kenya au mjini Hague. Wanasiasa walihujumu juhudi zote za kubuniwa kwa mahakama maalum nchini Kenya na hivyo Mahakama ya ICC ikaingilia kati.
Katika miezi ya hivi karibuni, mashahidi kadhaa wametishwa, na ICC imewaondoa baadhi ya mashahidi hao nchini humo.
Swala kuu ni iwapo wale watakaotajwa watajisalimisha wenyewe kwa mahakama ya ICC au watalindwa kisiasa na kuukwepa mkono wa sheria.

0 comments:

WELCOME URARY95 SPORTS NEWS BLOG | ADVERTISE YOUR BUSINESS HERE AT A CHEAP PRICE MORE INFORMATION CONTACT US: 0654315901 | Email: urary95@yahoo.com | KARIBU URARY95 SPORTS NEWS BLOG | TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA GHARAMA NAFUU KWA MAELEZO ZAIDI WASILIANA NASI: 0654315901 | Barua Pepe: urary95@yahoo.com
 
Back to top!