Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa- FAO, linasema maendeleo endelevu hayawezi kufikiwa  hadi pale njaa na utapia mlo zitakapotokomezwa. Katika ripoti iliyotolewa Jumatano  mkuu wa shirika hilo la FAO Jose Graziano da Silva, alisema lengo la maendeleo  endelevu kamwe haliwezi kufikiwa ikiwa takriban mmoja kati ya watu saba duniani anakabiliwa na njaa au utapia mlo . Alitoa mwito wa kuongeza  uzalishaji wa chakula na wakati huo huo kulinda mazingira ili dunia iweze kukidhi mahitaji ya chakula kwa watu wanaokisiwa kufikia bilioni tisa  ifikapo mwaka wa 2050. FAO linasema kufanikisha lengo hilo lazima uwezekazji katika kilimo uongezwe kwa asili mia 60 katika miongo ijayo. Shirika hilo linaongeza kuwa robo tatu ya watu maskini duniani huishi vijijini ambapo wengi wanategemea kilimo kwa maisha yao. Ripoti  ya shirika  hilo la FAO imetolewa kabla ya mkutano ujao wa Umoja wa Mataifa  unaotazamiwa kufanyika mjini Rio De Janeiro kuanzia Juni 20 hadi 22. Mchumi wa ngazi ya juu wa shirika  hilo la chakula na kilimo duniani aliiambia sauti ya Amerika kuwa ajenda kuu ya  mkutano huo itakuwa kutokomeza njaa duniani.