HOTUBA
YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI BUNGENI NDUGU KABWE ZUBERI ZITTO
(MB), WIZARA YA FEDHA NA UCHUMI, KUHUSU MAPENDEKEZO YA MAKADIRIO YA
MAPATO NA MATUMIZI YA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013
______________________
I. UTANGULIZI
Mheshimiwa
Spika, kwa niaba ya Kambi ya Upinzani, ninatoa maoni ya Kambi ya
Upinzani kuhusu Bajeti ya Nchi ya mwaka wa fedha 2012/2013 kwa mujibu wa
Kanuni za Bunge Kifungu cha 99(7) toleo la Mwaka 2007.
Mheshimiwa
Spika, Natoa pongezi za dhati kabisa kwa Ndugu William Augustao Mgimwa,
Mbunge wa Jimbo la Kalenga mkoani Iringa kwa kuteuliwa na Rais kuwa
Waziri wa Fedha na Uchumi. Vile vile nawapongeza Ndugu Saada Mkuya na
Ndugu Janeth Mbene kwa kuteuliwa kwao kuwa Wabunge na baadaye kuwa
Manaibu Mawaziri katika Wizara hii nyeti sana. Ninawapa pole pia maana
Wizara ya Fedha sio Wizara lelemama. Kambi ya Upinzani itaendelea
kuisimamia Wizara hii kwa ukaribu sana kama ilivyofanya katika kipindi
cha miaka miwili iliyopita. Mtakapofanya vizuri tutawapongeza ili
muongeze juhudi, mtakapoharibu tutawawajibisha.
Mheshimiwa
Spika, Ni dhahiri kwamba Mwaka wa Fedha uliopita ulikuwa mwaka mgumu
sana kwa Watanzania. Ni mwaka ambao gharama za maisha zilipanda kwa kasi
kubwa sana na juhudi za Serikali kuwakwamua wananchi na hasa wananchi
wanyonge kutoka kwenye lindi la ufukara ziligonga mwamba. Kambi ya
Upinzani inawapa pole Watanzania kwani hili ndilo walilochagua. Muhimu
ni kuvumilia mpaka uchaguzi ujao na kufanya mabadiliko ya Serikali ili
kuweka Serikali itakayoongozwa na CHADEMA na itakayoweza kukabili
changamoto za sasa na za baadaye.
Mheshimiwa Spika, naomba tufanye mapitio kidogo ya Bajeti inayomaliza muda wake.
UTEKELEZAJI WA BAJETI ILIYOPITA
Mheshimiwa
Spika, kabla ya kutoa bajeti mbadala ya Kambi ya Upinzani ni vema
kufanya tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya Serikali iliyopita ili
kuona ni kwa namna gani Serikali inathamini fedha za walipa kodi, na
dhamira yake ya kuleta maendeleo ya kiuchumi katika Taifa. Katika
kufanya hivyo, tutapitia baadhi ya maeneo ambayo Kambi ya Upinzani
tunaona kuwa hayakutekelezwa katika bajeti iliyopita.
Kupunguza Makali ya Maisha
Mheshimiwa
Spika, Katika Bajeti ya mwaka 2011/12 Serikali ilitangaza nia yake ya
kupunguza makali ya maisha. Hatua mbali mbali zilichukuliwa ikiwamo
kupunguza kodi na tozo kwenye mafuta ya Dizeli na Petroli, kuanza
kutekeleza mpango wa dharura wa umeme na kutoa fedha za kununua chakula
kwa Wakala wa Chakula. Serikali ilitumia shilingi bilioni 296 na dola za
Marekani milioni 183 kwenye Umeme. Vilevile Serikali ilitumia shilingi
bilioni 27 kununua Mahindi na kusambaza kwenye masoko.
Mheshimiwa
Spika, licha ya hatua hizo zilizochukuliwa Mfumuko wa Bei uliongezeka
maradufu kutoka wastani wa asilimia 6.3 mwaka 2010/11 mpaka wastani wa
asilimia 17.8 mwaka 2011/12. Serikali imefeli katika lengo lake la
kupunguza makali ya maisha kwa wananchi. Sio tu kwamba Serikali
imeshindwa kudhibiti upandaji holela wa gharama za maisha bali pia hatua
za Serikali zimeongeza kasi ya kupanda kwa makali ya maisha.
Mheshimiwa
Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni katika Hotuba yake mbadala ya mwaka
2011/12 iliitaka Serikali kushughulikia msingi wa mfumuko wa Bei hapa
nchini ambao ni uzalishaji mdogo wa mazao ya chakula. Tumeelezwa na
Waziri Kivuli wa Mipango na Uchumi kwamba Chakula peke yake ni asilimia
48 ya kapu la bidhaa na huduma ambazo mwanachi anatumia. Mfumuko wa Bei
ya Chakula kinacholiwa nyumbani na kwenye migahawa ilikuwa asilimia 25
mwezi Aprili 2012 (BoT monthly Economic Review, May 2012). Vile vile
mfumuko wa bei wa nishati inayotumika nyumbani na mafuta ya Dizeli na
Petroli ulifikia asilimia 25 pia mwezi Mei mwaka 2012. Ni dhahiri kwamba
iwapo tutadhibiti mfumuko wa bei ya chakula tutaweza kushusha mfumuko
wa bei kurudi kwenye tarakimu moja.
Mheshimiwa
Spika, Serikali inapendekeza hatua zilezile ilizofanya mwaka wa fedha
unaokwisha kwa kutoa vibali kwa Wafanyabiashara vya kuagiza Mchele na
Sukari. Katika hotuba yake Waziri wa Fedha anasema ‘….Serikali ilitoa
vibali vya kuagiza sukari bila kutoza ushuru wa forodha kiasi cha tani
200,000 ili kukabiliana na uhaba na kupanda kwa bei ya Sukari…’(uk 9
ibara ya 15). Baada ya hatua hii bei ya Sukari ilipanda kutoka tshs
1700 mpaka tshs 2800 kwenye maeneo mengi nchini. Waziri wa Fedha katika
hotuba yake anatoa suluhisho. Ninanukuu. ‘…hatua za haraka ambazo
Serikali itachukua ni pamoja na kutoa vibali vya uagizaji wa Sukari na
mchele kutoka nje….’! Serikali inachukua hatua zilezile kwa tatizo lile
lile ikitegemea matokeo tofauti.
Mheshimiwa
Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni inarejea pendekezo lake la mwaka jana
kwa Serikali kutoa vivutio kwa wakulima wadogo kuzalisha chakula kwa
wingi. Miongoni mwa vivutio hivyo ni:
Kuwekeza kwenye barabara za vijijini ili mazao yao yafike kwenye masoko na kupata bei nzuri,
Kuwekeza
kwenye Usambazaji wa Maji vijijini ili kina mama wasitembee mwendo
mrefu kutafuta maji na hivyo kutumia muda mwingi kwenye uzalishaji,
Kuwekeza
kwenye Umeme vijijini ili wafanyabiashara wa vijijini waongeze thamani
ya mazao. Kwa mfano, kuuza Unga badala ya Mahindi.
Kuwekeza kwenye miundombinu ya Umwagiliaji vijijini ili wakulima wazalishe muda wote wa mwaka.
Kuwekeza
kwenye Elimu vijijini na pia Afya vijijini ili wananchi wetu wawe na
Afya bora na waelimike katika mbinu za uzalishaji bora.
Mheshimiwa
Spika, Kambi ya Upinzani inaamini kuwa, hakuna mbadala wa kudhibiti
mfumuko wa bei zaidi ya kuongeza uzalishaji wa chakula na kuwekeza kwa
wananchi wetu. Serikali inafikiria uzalishaji utaongezeka kwa kusaidia
wakulima wakubwa ambao watageuza wananchi wetu kuwa Manamba na vibarua
ndani ya nchi yao. Tuwekeze kwa watu wetu vijijini ili waongeze
uzalishaji na kwa kufanya hivyo mfumuko wa Bei ya chakula utakuwa
historia. Hakuna mwarobaini wa kupanda kwa bei za vyakula isipokuwa
Kilimo.
Mhesimiwa
Spika, Tunatambua kuwa hatua tunazotaka Serikali ifanye ni za muda wa
kati. Kwa muda mfupi tunataka Bodi ya Mazao mchanganyiko, Wakala wa
Hifadhi ya Chakula na Bodi ya Sukari zipewe fedha kuagiza Mchele na
Sukari na pia kununua kutoka kwa wakulima na kusagisha Mahindi.
Wafanyabiashara waagizaji wa Chakula washindane na Taasisi hizi za Umma
badala ya kuwapa vibali ambavyo hutolewa kwa rushwa na hivyo kuongeza
bei za bidhaa hizo.
Kuwezesha Wananchi Kiuchumi na Kuongeza Ajira.
Mheshimiwa
Spika, Serikali imesema kwamba ilichukua hatua mbalimbali kukabiliana
na tatizo la Ajira kwa kuongeza fursa za ajira. Miongoni mwa hatua
zilizochukuliwa ni pamoja na kuongeza mitaji katika Benki ya Rasilimali,
Benki ya Wanawake, Benki ya Posta na Twiga Bancorp. Pia Serikali
imetangaza kwamba imeajiri walimu, maafisa ugani na watumishi wa Afya.
Hatua kama hizi pia zimetangazwa kwa mwaka wa Fedha wa 2012/13 ambapo
pia Serikali imetangaza kuajiri watumishi 71,756.
Mheshimiwa
Spika, Duniani kote Serikali haizalishi ajira bali ajira huzalishwa na
Uchumi mzima ambapo Serikali ni sehemu tu ya Uchumi (Jobs are created by the economy).
Takwimu zinaonyesha kwamba kila mwaka Tanzania inaingiza kwenye soko la
Ajira watu takribani laki saba. Shughuli za Uchumi zikiongezeka ndio
Ajira zinatengenezwa. Serikali inafikiria nini kuhusu vijana takribani
milioni nane walio shule za Msingi hivi sasa, Vijana milioni 1.7 walio
katika Shule za Sekondari hivi sasa, Vijana 200,000 waliopo vyuo vya
Ufundi na Wanachuo 180,000 walio katika Vyuo vya Elimu ya Juu (takwimu
kutoka kitabu cha hali ya uchumi, 2012 sura ya 19). Serikali ambayo bado
inategemea takwimu za Ajira za Mwaka 2006 inajitamba kwa kuajiri watu
70,000.
Mheshimiwa
Spika, Jukumu la Serikali ni kujenga mazingira ya wananchi kupata ajira
ama kwa kujiajiri au kwa kuajiriwa na shughuli za uchumi. Lakini ukweli
ni kwamba Serikali imeshindwa kushughulikia tatizo la Ajira na hasa
ajira kwa vijana. Tatizo la Ajira kwa Vijana ni Bomu litakalokuja
kutulipukia vibaya sana kama hatutakuwa makini nalo. Hii ni nchi ya
Vijana. Kutoshughulikia masuala yao ni kutoshughulikia masuala ya nchi.
Mheshimiwa
Spika, changamoto ya ajira kwa vijana Bajeti mbadala imeiwekea mikakati
mipana ya kiuchumi kwa kuanzisha miradi mikubwa ya Umma itakayomeza
vijana waliopo mtaani na kuanzisha kwa makusudi na kwa kasi Vyuo vya
Ufundi stadi na Vyuo vya Ufundi na Mafunzo vingi. Kambi ya Upinzani
Bungeni inapendekeza Uwekezaji wa Miundombinu Vijijini kama njia ya
kupunguza tatizo la ajira kwa vijana. Vilevile tunapendekeza Miradi
mikubwa ya kuongeza mazao ya Kilimo hasa Pamba, Korosho na Katani ili
kupanua Ajira. Kambi ya Upinzani pia inapendekeza kujenga VETA katika
kila Halmashauri ya Wilaya na Chuo cha Ufundi katika kila Mkoa ili kutoa
ujuzi kwa vijana ili waweze kukabili maisha yao. Badala ya Serikali
kukopa kwa ajili ya Matumizi ya kawaida, Serikali ikope kujenga Vyuo vya
Ufundi Stadi na vyuo vya Ufundi na Mafunzo. Ni Lazima viongozi sio tu
tuwe makini bali tuonekane kuwa makini tunaposhughulikia suala la Ajira
kwa Vijana.
Sera ya Mapato
Mheshimiwa
Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni ilitangaza vipaumbele katika sera ya
Mapato ambavyo ni pamoja na kukusanya Mapato ya Serikali mpaka zaidi ya
asilimia 20 ya Pato la Taifa ili kuwezesha kujitegemea kupata fedha za
miradi ya maendeleo. Pia Kambi ya Upinzani inakusudia kufanya
marekebisho mbalimbali ya sheria za kodi ili kulinda viwanda vya ndani
vinavyotumia malighafi za kilimo na mifugo za hapa nchini, kupanua wigo
wa Mapato kwa kutunga sheria ya kulazimu kila Mtanzania kujaza fomu za
marejesho ya kodi na kurekebisha viwango vya kodi ya Mapato (PAYE). Vile
vile tunapendekeza kufanya marekebisho ya sheria za kodi kwenye sekta
za madini na mawasiliano ili kuongeza mapato ya Serikali.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa Fedha 2011/12 Serikali ilichukua hatua
mbalimbali katika masuala ya Kodi. Katika Bajeti mbadala pia
tulipendekeza hatua mbali mbali ambazo tuliona zitaongeza mapato ya
Serikali na hivyo kutuwezesha kuendeleza nchi yetu. Baadhi ya hatua
mbalimbali tulizopendekeza Serikali imetangaza kuzitekeleza.
Mheshimiwa
Spika, Kambi ya Upinzani katika Bajeti Mbadala ya mwaka 2011/12
ilipendekeza masuala yafutayo ili kuongeza mapato ya Serikali.
Hatua
zifuatazo zilipendekezwa ili kuweza kukabiliana na ukwepaji wa kodi
unaofanywa na makampuni makubwa ya kimataifa (Multinational
Corporations) na hatimaye kulipunguzia taifa mapato:
Kutunga
sheria kwa kuimarisha zaidi sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004
kwamba, mikopo ya makampuni kwenye uwekezaji, kwa sababu za kikodi,
isizidi asilimia 70 ya mtaji wote uliowekezwa na hii ianze mara moja
bila kujali mikataba iliyopo.
Kutunga
sheria kuhakikisha kwamba riba kwenye mikopo kutoka Makampuni
yanayohusiana (sister companies) haitaondolewa kwenye kutoza kodi (not
tax deductible).
Kuhakikisha
kwamba mauziano ya Kampuni yoyote ambayo mali zake zipo Tanzania
yanatozwa kodi ya asilimia 30% kama ‘ongezeko la mtaji’ (‘capital
gains’).
Mheshimiwa
Spika, katika mapendezo haya ni pendekezo moja tu ndilo limechukuliwa
na Serikali katika Bajeti ya mwaka 2012/13 nalo ni pendekezo la ‘capital
gains tax’. Hata hivyo Pendekezo la Serikali lina makosa makubwa sana
ya kifundi. Waziri wa Fedha Mhe. Mgimwa amesema, ninanukuu ‘Kuanzisha
kodi itokanayo na uuzaji wa rasilimali ya uwekezaji (capital gains tax)
kwenye uuzaji wa HISA za kampuni mama ya nje ya nchi’
Mheshimiwa
Spika, Ukisoma pendekezo letu kwa haraka utaona kama Serikali
imelichukua lilivyo, lakini kwa jicho la kiuchumi pendekezo la Serikali
na lile la Kambi ya Upinzani ni mambo tofauti sana. Pendekezo la
Serikali linazungumzia HISA. Mamlaka ya Mapato Tanzania haitakuwa na
mamlaka (jurisdiction to tax) kutoza kodi kwa Kampuni mama (as a source
or even residence). Mamlaka ya Mapato Tanzania ina mamlaka na Mali
(assets) zilizopo Tanzania za Kampuni mama. Kwa mfano, wakati kampuni ya
Barrick inanunua mgodi wa Bulyanhulu haikuinunua Kampuni ya Kahama
mining ltd bali ilinunua hisa zote za Kampuni ya Sutton Resources. Vile
vile, wakati Zain inanunua Celtel, haikununua Celtel Tanzania ltd bali
Celtel Africa BV ambayo ilikuwa inamiliki Celtel Tanzania BV ambayo
ilimiliki Celtel Tanzania ltd. Hivyo hivyo ilikuwa kwa AirTel
ilipoinunua Zain. Kukwepa mitego hii ya Mashirika ya Kimataifa (MNCs)
sheria itaje kwamba Kodi hii itozwe kwa Mali zilizopo Tanzania na sio
kwa HISA kama alivyopendekeza Waziri wa Fedha. Hata hivyo Kambi ya
Upinzani inatambua hatua hiyo ya Serikali kuchukua wazo hili ili
kuongeza Mapato ya nchi.
Misamaha ya Kodi
Mheshimiwa
Spika, Katika Bajeti ya mwaka 2011/12 Serikali iliahidi kupunguza
misamaha ya Kodi mpaka kufikia asilimia 1 ya Pato la Taifa. Ahadi hii
haikutekelezwa na Serikali na badala yake imerejea kuahidi tena. Waziri
wa Fedha ameliambia Bunge katika hotuba yake, nanukuu ‘kuendelea kufanya mapitio ya sharia mbalimbali zinazotoa misamaha ya kodi kwa lengo la kudhibiti na kupunguza misamaha hiyo’
(uk.39). Badala ya Serikali kutuambia hivi sasa misamaha ya kodi
imefikia asilimia ngapi, imeendelea kutoa ahadi isizoweza kutekeleza.
Mheshimiwa Spika, Katika Taarifa ya Utafiti uliofanywa na Jopo la Taasisi za dini hapa nchini waliyoiita ‘The One Billion Dollar Question’
imeonekana kwamba Tanzania inapoteza takribani shilingi trilioni 1.7
kutokana na misamaha ya kodi, ukwepaji wa kodi, utoroshaji wa mitaji nje
na udanganyifu katika biashara ya kimataifa. Fedha hizi ni zaidi ya
jumla ya Bajeti za Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Nishati na Madini.
Fedha hizi ni zaidi ya Mkopo ambao Serikali itadhamini kwa TPDC ili
kujenga Bomba la Gesi kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam. Fedha hizi
zinazopotea kutokana na misamaha ya kodi ni zaidi ya gharama za Ujenzi
wa Gati mpya katika Bandari ya Dar es Salaam. Kambi ya Upinzani
inawapongeza Viongozi wa Dini kwa kufanya kazi hii nyeti sana lakini
tunampongeza zaidi Mtafiti Mtanzania Dokta Prosper Ngowi kwa kushiriki
katika utafiti huu. Tunaishauri Serikali kusoma Taarifa hii na
kutekeleza mapendekezo yake ili kuongeza mapato ya Serikali. Lugha za
kufanya mapitio kila mwaka hazisaidii, wananchi wanataka kuona misamaha
ya kodi imepungua mpaka kiwango kinachostahili cha asilimia 1 ya Pato la
Taifa.
Kurekebisha mfumo wa Kodi ya Mapato
Mheshimiwa
Spika, Bajeti mbadala ya mwaka 2011/12 ilipendekeza kuifanyia
marekebisho sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004. Tunarejea pendekezo
letu na kuongeza pia kwamba sehemu ya kodi ya Mapato inayotoa fursa
(grandfathering) kwa Kampuni za Madini kutumia sheria ya kodi ya Mapato
iliyofutwa ya mwaka 1973, ifutwe. Pendekezo letu lina lengo la kutaka
kuweka mfumo wa ‘straightline method of depreciation’ ya asilimia 20
badala ya sasa ambapo Kampuni za Madini hufanya ‘100% depreciation’
kwenye Mitambo yao mwaka wa kwanza na hivyo kuchelewesha kulipa
‘Corporate Tax’.
Mheshimiwa
Spika, Serikali imeamua kupandisha kiwango cha chini cha kipato ili
kutoza kodi ya Mapato (PAYE) kutoka tshs 135,000 mpaka tshs 170,000 bila
kushusha kodi yenyewe. Hii haitamsaidia mwananchi hata kidogo kwani
bado kiwango cha kodi cha asilimia 14 kipo juu sana. Vile vile kiwango
cha chini cha pato litakalotozwa kodi kitawaathiri wafanyakazi wa
Serikali maana ndio ambao Serikali ina mamlaka ya kutangaza kima cha
chini cha Mshahara wao na kuwaacha wafanyakazi wa Sekta Binafsi ambao
wengi hulipwa kiwango kidogo sana cha mishahara. Kimsingi kutokana na
tangazo lake, Waziri wa Fedha ametangaza kima kipya cha chini cha
mshahara kuwa kitakua tshs 170,000.
Mheshimiwa
Spika, tunarejea kauli yetu kwamba kupanda kwa gharama za maisha
kumepunguza uwezo wa matumizi ya wananchi walioajiriwa na kulipwa
mishahara ambayo inakatwa kodi (PAYE). Tunapendekeza kwamba PAYE ianzie
asilimia 9 kutoka asilimia 14 na kiwango cha chini cha kutoza kiwe tshs
150,000. Tunatambua kuwa kodi hii ni chanzo kikubwa cha Mapato kwa
Serikali ambapo kwa mwaka huu wa Fedha kinatarajiwa kuingiza takribani
shilingi bilioni 1,437 (asilimia 18 ya Mapato yote ya kodi
yanayokusanywa na TRA) kutoka Idara ya Kodi za Ndani (Wafanyakazi wa
Serikali tshs 115bn, Wafanyakazi wa Mashirika ya Umma tshs 47bn na
Wafanyakazi wa Sekta binafsi tshs 312bn) na Idara ya Walipa kodi wakubwa
(Wafanyakazi wa Serikali tshs 450bn, Wafanyakazi wa Mashirika ya Umma
Tshs108bn na Wafanyakazi wa Sekta Binafsi tshs 406bn). Hata hivyo
wananchi wanapobakia na pesa za matumizi kodi nyingine kama VAT na
Ushuru wa Bidhaa huongezeka na hivyo kupunguza kiwango cha Mapato ya
Serikali ambayo yangepotea kutokana na uamuzi huu.
Mheshimiwa Spika, Hata hivyo bado kuna haja ya kuangalia upya ‘tax brackets’ na kuzirahisisha kwa kuzipunguza na kuongeza kiwango cha kodi ya Mapato kwa watu wenye kipato kikubwa zaidi.
Mheshimiwa
Spika, ili kuongeza mapato kutoka kwa watu wenye kipato kikubwa kambi
ya Upinzani inapendekeza mabadiliko katika viwango vya juu vya kodi ya
Mapato ambapo tunapendekeza kupandisha kiwango cha juu kabisa cha
kukokotoa kodi ya mapato (PAYE) kiwe shilingi milioni kumi na kodi iwe
asilimia 42 kutoka asilimia 30 ya sasa.
Mheshimiwa
Spika, Tunapendekeza kwamba mtu yeyote anayepata mapato ya zaidi ya
shilingi 10,000,000 alipe kodi ya Mapato ya shilingi 500,000 kujumlisha
na asilimia 42 ya tofauti ya shilingi 10,000,000 na shilingi 3,200,000
kama inavyoonekana kwenye jedwali hapa chini. Lengo la mapendekezo haya
ni kuwafanya watu wenye kipato kikubwa walipe kodi zaidi kulingana na
kipato wanachopata maana hivi sasa masikini wanalipa kodi nyingi zaidi
kuliko wenye nacho.
Mapato ya kutozwa kodi kwa mwezi
|
Kodi (PAYE)
|
Mapendekezo ya mapato ya kutozwa kodi kwa mwezi
|
Kiwango kipya cha Kodi (PAYE)
|
Mapato yanayozidi shilingi 720,000
|
Sh. 112,500 ongeza 30% ya kiasi kinachozidi sh. 720,000
|
Mapato yanayozidi 720,000 lakini hayazidi sh. 3,199,199
|
Sh.112,500 ongeza 30% ya ziada ya sh. 720,000
|
Mapato yanayozidi sh. 3,200,000 lakini hayazidi sh.9,999,999
|
Sh.190,000 ongeza 38% ya ziada ya 3,200,000.
| ||
Mapato kuanzia sh. 10,000,000 na kuendelea
|
Sh. 500,000 ongeza 42% ya mapato yake.
|
Mheshimiwa
Spika, Mapendekezo haya hayatapunguza Mapato ya Serikali kwani wigo wa
kodi utakuwa umeongezeka kwa kuwagusa wafanyakazi katika sekta binafsi
na pia kupata kodi zaidi kutoka kwa watu wenye kipato kikubwa zaidi.
Mheshimiwa
Spika, vile vile Kambi ya Upinzani inaendelea kupendekeza kuwa mchakato
uanze ili kila Mtanzania mwenye umri wa miaka 18 na zaidi awe anajaza
fomu za kodi (tax returns) kila mwaka. Suala hili ni muhimu sana na
litangazwe mwaka huu ili tuwe na mwaka mzima wa kujitayarisha ili lianze
Mwezi Julai mwaka 2013. Mtanzania yeyote, awe na kipato au asiwe na
kipato ajaze Tax Returns. Mfumo huu utatoa takwimu muhimu sana kwa
Mamlaka ya Mapato Tanzania na utasaidia sana hapo baadaye kupanua wigo
wa Mapato. Tunapendekeza marekebisho katika Sheria ya Kodi ya Mapato ili
mfumo huu uwepo kisheria ndani ya mwaka mmoja kuanzia sasa.
Mheshimiwa
Spika, Vile vile, Kambi ya Upinzani inapendekeza kuanzishwa kwa Real
Estate Regulatory Authority kama tulivyofanya kwa mwaka uliopita na
kwamba kila mwenye nyumba ya kupangisha lazima atambuliwe na kulipa kodi
inavyostahili. Lengo ni kuhakikisha Sekta ya Nyumba inatoa mapato ya
kutosha kwa Serikali na kuzuia mianya ya ukwepaji kodi inayofanywa na
wenye nyumba.
Presumptive Tax
Mheshimiwa
Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni ilipendekeza mwaka 2011/12 kwamba
ushauri wa Mradi wa kuboresha mfumo wa kodi (Tax Modernisation Project)
ambao ulishauri kwamba ipo haja ya kuainisha Kodi ya VAT na Presumptive
Tax, utekelezwe. Tunashauri kuwa kodi anayotozwa mfanyabiashara
ndogondogo kabla hajaanza kufanya biashara ifutwe kabisa. Uamuzi huu
utapunguza mapato ya Serikali (Shilingi bilioni 21.6 kwa mujibu wa
Kitabu cha Bajeti Vol. I) katika kipindi cha muda mfupi lakini itakuwa
ni chanzo kikubwa sana cha mapato katika kipindi cha muda mrefu.
Vyanzo vipya vya Mapato
Mheshimiwa
Spika, Pamoja na kupitia vyanzo vya mwaka jana na kulinganisha na
mapendekezo ya Serikali, Kambi ya Upinzani bado inapendekeza vyanzo vya
ziada mwaka huu ili kuboresha Mapato ya Serikali.
Kupanua wigo wa Skills Development levy
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani tunapenda kushukuru kuwa wazo letu la kutoza kodi ya skills development levy
tuliyopendekeza katika hotuba yetu ya mwaka uliopita lilifanyiwa kazi
na serikali lakini kwa mwaka ujao wa fedha tunaitaka serikali kuipitia
upya kodi kwa kuongeza wigo wa wachangiaji ili kuwa na fedha za kutosha
kwa ajili ya kugharamia elimu ya juu.
Mheshimiwa Spika, tunapendekeza kiwango cha tozo ya kuendeleza stadi (skills development levy – SDL) kishuke
kutoka asilimia 6 ya sasa mpaka asilimia 4. Tunapendekeza kuwa Waajiri
wote walipe kodi hii ikiwemo Serikali na Mashirika ya Umma. Lengo ni
kupunguza mzigo kwa Waajiri na kuondoa ubaguzi kwani wanaofaidika na
tozo hii (wanafunzi wa elimu ya Juu) pia huajiriwa na Serikali na
Mashirika ya Umma. Serikali ilipanga kukusanya tshs 161bn kutoka katika
tozo hii kwa mfumo wa sasa.
Mheshimiwa Spika, Marekebisho ambayo Kambi ya Upinzani inayapendekeza yataongeza mapato ya Serikali mpaka tshs 320bn.
Mheshimiwa
Spika, Waziri wa Fedha katika tozo hii amesema Serikali ‘itapitia upya
maudhui ya viwango vya tozo’ hii. Kambi ya Upinzani imetamka maudhui na
viwango na tunaiomba Serikali itekeleze pendekezo hili.
Mheshimiwa
Spika, Tunapendekeza mgawanyo wa tozo hii urekebishwe kwa kuongeza
mapato yatakayokwenda kwenye Vyuo vya Ufundi mchundo.
Mheshimiwa
Spika, kama wanafunzi wetu watasomeshwa na kodi hii basi tuangalie upya
mfumo wa Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu. Fedha inayopatikana
kwenye Kodi hii itumike kusomesha kwa ‘grant’ wanafunzi wanaofanya
vizuri zaidi darasani na kuwapunguzia mzigo wa mikopo. Vile vile
tuangalie kama tunaweza kukopesha wanafunzi malazi na chakula tu na
kutoa bure ada na mafunzo kwa vitendo pamoja na vitabu.
Kulinda kazi za Wasanii
Mheshimiwa
Spika, Kambi ya Upinzani mara kwa mara tumekuwa tukieleza jinsi wasanii
wanavyoshindwa kunufaika na kazi zao kutokana na kukosekana mfumo rasmi
wa kiserikali unaozuia wizi wa kazi za wasanii. Pamoja na serikali
kukubali kuahidi kuwa na mfumo rasmi wa kuzuia wizi wa kazi hizo,
serikali haijaweka wazi mfumo rasmi utakaokuwa unatumika kuzuia wizi huo
na hatimaye wasanii kunufaika na kazi zao.
Mheshimiwa
Spika, Kambi ya upinzani katika hotuba ya Wizara ya Habari Vijana na
Michezo kwa mwaka uliopita tulingumzia suala hili na tulishauri kwamba
kuwe na utaratibu wa kuweka sticker maalumu zinazotolewa na
mamlaka za serikali kuonyesha uhalali wa muuzaji wa kazi za wasanii.
Serikali imetekeleza pendekezo letu. Hata hivyo tuna maoni tofauti
kuhusu namna ya kutekeleza pendekezo hili.
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo, serikali mwaka 2006 kupitia
gazeti la Serikali Na. 18 la tarehe 10 Mwezi wa Februari, ilianzisha
utaratibu wa HAKIGRAM kama stiker maalumu za kazi halali za wasanii
zinazotolewa na COSOTA. Kambi ya Upinzani tunapendekeza utaratibu huo
uendelee na Mamlaka ya Mapato TRA ihusike kukusanya mapato kwa ajili ya
kazi hiyo na COSOTA wataratibu utoaji wa HAKIGRAM. Hii itaenda
sambasamba na kuzuia uchakachuaji wa HAKIGRAM hizo ili kutopoteza lengo
la kuweka mfumo huo. Stiker zisitolewe na TRA bali zitolewe na COSOTA na
TRA isimamie eneo la Mapato tu. Hii itasaidia kwani stiker hizi
hazitatumika kupata mapato peke yake bali pia kuweka kumbukumbu muhimu
za kazi za wasanii.
Mapato kutoka Sekta ndogo ya Mawasiliano ya Simu
Mheshimiwa
Spika, serikali imekuja na pendekezo la kuendelea na kutoza ushuru wa
bidhaa kwenye masuala ya huduma ya mawasiliano ya simu, jambo ambalo
litamgusa mtumiaji wa huduma hiyo ambaye ni mwananchi wa kawaida na
hivyo kuongeza gharama za simu. Kambi ya Upinzani inapinga kabisa
kuongeza ushuru wa bidhaa kwenye muda wa Maongezi (airtime) kwenye simu
za mkononi.
Mheshimiwa
Spika, Hoja ya wananchi hapa ni kwamba Kampuni za Simu za mkononi
hazilipi kodi ya kutosha na hasa kodi ya Makampuni (corporate tax).
Waziri Mkuu alipokuwa anafunga Bunge la Bajeti mwaka 2011 alitangaza
Kampuni ambazo ni walipa kodi wakubwa katika kipindi cha miaka 5
iliyopita. Katika orodha hiyo kulikuwa na Kampuni moja tu ya Simu za
Mkononi (Kampuni ya AirTel).
Mheshimiwa
Spika, wakati wananchi wanataka kodi zaidi kutoka Kampuni za simu,
Serikali inapendekeza kuongeza kodi kwa mwananchi anayetumia simu.
Kampuni zilipe kodi ya Mapato na sio kukandamiza wateja kwa ushuru wa
bidhaa ilihali huduma zenyewe za simu hazina ubora.
Mheshimiwa
Spika, vilevile wananchi wanalalamika kwamba Kampuni za simu za Mkononi
hajiweki wazi mapato yake yote hali iliyopelekea Kamati ya Bunge ya
POAC kuiagiza TCRA kufunga mtambo utakaoweza kuijulisha TCRA mapato yote
ambayo kampuni za Simu zinapata. Serikali ya Ghana ilifanya hivi na
kupandisha maradufu mapato yanayotokana na sekta ndogo ya simu. Hivi
sasa Ghana, nchi yenye watumiaji wa simu milioni 17 ukilinganisha na
Tanzania yenye watumiaji 23 milioni, inakusanya asilimia 10 ya Mapato ya
Serikali kutoka kwenye kampuni za Simu peke yake. Iwapo Tanzania
ikifikia kiwango cha Ghana cha asilimia 10 ya Mapato ya ndani ya
Serikali kutoka kwenye kampuni za simu, Tanzania itaweza kukusanya zaidi
ya Shilingi bilioni 860 kutoka kwenye sekta ndogo ya simu peke yake.
Hata hivyo mazingira ya Ghana na Tanzania ni tofauti na hivyo
tunapendekeza kiwango kutokana na hali yetu.
Mheshimiwa
Spika, Shirika la TCRA kupitia zabuni nambari AE-020/2010-11/C/04
imetangaza ‘request for expression of interest for design, development,
installation and Management of Telecommunication monitoring system under
build, operate and transfer’ ili kupata chombo cha kufuatilia Mapato ya
Kampuni za Simu. Kwa mujibu wa ratiba zilizotangazwa na TCRA chombo
kitakuwa kimeanza kazi mwishoni mwaka huu wa 2012. Kwa dhati kabisa
napenda kumpongeza Mkurugenzi Mkuu wa TCRA na watumishi wote kwa
kutekeleza maelekezo ya Kamati ya Bunge kwa haraka ili kuhakikisha
mapato kwa nchi yetu.
Mheshimiwa
Spika, kilichotushangaza ni kwamba Waziri wa Fedha na Uchumi hakugusia
kabisa suala hili muhimu sana kwa mapato ya Serikali badala yake
Serikali imekimbilia kukandamiza wanyonge watumiaji wa Simu na kuyaacha
Makampuni ya Simu yakilipa kiduchu kutoka kwenye mapato yao.
Mheshimiwa
Spika, uamuzi huu wa kufuatilia mapato ya Kampuni za Simu na
Marekebisho tunayopendekeza ya kujenga uwezo zaidi wa TCRA kwa kuwa na
Idara ya ‘Revenue Assurance’ na kurekebisha sheria ya TCRA kwa kuweka
wazi makujumu ya TRA ndani ya TCRA, utaiingizia Serikali mapato ya
takribani tshs 660bn.
Mheshimiwa
Spika, katika eneo hili la Sekta ya Mawasiliano ninaomba kurejea
kuitaka Wizara ya Fedha itoe maelezo hapa Bungeni namna ambavyo Hisa za
serikali katika Kampuni ya MIC Tanzania ltd inayomiliki Kampuni ya Tigo
zilivyouzwa. Mheshimiwa Spika Serikali ilikuwa inamiliki hisa asilimia
26 katika Kampuni hii. Kwa mujibu wa kumbukumbu nilizoziona Hisa hizi
zote ziliuzwa kwa thamani ya dola laki saba kwa mwana hisa mwenza mnamo
mwezi Februari mwaka 2004. Kampuni hii leo inapata mapato ya Tshs
bilioni 20 kwa mwezi, tuliuza hisa zetu asilimia 26 kwa dola laki saba!
Laki Saba dola! Kambi ya Upinzani inataka uchunguzi maalumu katika mauzo
haya na Taifa liambiwe nini kilitokea na hatua gani za kuchukua dhidi
ya waliouza mali hii ya Umma bila zabuni wala kuzingatia thamani ya
fedha.
Kuzuia mauzo ya ngozi ghafi nje ya nchi
Mheshimiwa
Spika, Kambi ya Upinzani imeshangazwa na hatua ya serikali kuja na
pendekezo la kuongeza ushuru kwenye bidhaa ya ngozi ghafi
inayosafirishwa nje kutoka asilimia 40 hadi 90 lengo likiwa ni
kuhamasisha usindikaji wa ngozi hiyo na kuiongezea thamani.
Mheshimiwa
Spika, kwa nchi iliyo na mianya mingi ya rushwa kama Tanzania hatua hii
haitakuwa na tija kwa kuwa wafanyabiashara wengi wa ngozi ghafi
wamekuwa na tabia ya kupunguza takwimu za kusafirisha ngozi ghafi na
hivyo kupelekea serikali kukosa mapato mengi sana. Serikali inafahamu
kwamba hata ushuru wa mauzo nje wa asilimia 40 haukuweza kutatua tatizo
la viwanda vya ndani kukosa malighafi. Kambi ya Upinzani haikubaliani na
Pendekezo la Serikali kwani halitatatua tatizo la kukuza sekta ndogo ya
Ngozi nchini.
Mheshimiwa
Spika, Kambi ya Upinzani tunaitaka serikali kuzuia kabisa kusafirisha
ngozi ghafi kwenda nje na badala yake kuwe na mpango wa kutumia ngozi
ghafi hapa nchini na kuleta tija katika uchumi wa taifa kwa kutengeneza
ajira na kuongeza thamani ya mauzo nje.
Mheshimiwa
Spika, hatua ya kuzuia ngozi ghafi kusafirishwa kwenda nje kwa Tanzania
itakuwa sio suala jipya kwa sababu Ethiopia imezuia na kuwekeza katika
kiwanda cha viatu, mikanda na bidhaa za ngozi. Kutokana na Mpango wa
Mendeleo ya Ethiopia (GTP – Growth and Transformation Plan) sekta ya
Ngozi itaingiza fedha za kigeni za thamani ya dola za Kimarekani bilioni
4 kwa mwaka. Hii ni sawa na fedha za kigeni ambazo Tanzania inapata
kutoka kwenye Dhahabu na Utalii kwa pamoja. Ethiopia nchi iliyokuwa
inatembea na bakuli na kulia njaa leo inakuwa nchi ya kupigiwa mfano na
sisi Watanzania! Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda pia amepiga
marufuku kuuza ngozi ghafi nje. Hata nchi ya Pakistani ambayo ndio ngozi
zetu zinakwenda nayo imepiga marufuku mauzo ya ngozi ghafi nje.
Serikali ipige marufuku Mauzo ya ngozi ghafi nje ya Nchi ili kulinda
viwanda vya ngozi nchini, kuoongeza Ajira na kuongeza mapato ya Fedha za
kigeni.
Kufuta Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa bidhaa za Maziwa
Mheshimiwa
Spika, sekta ndogo ya Maziwa hapa nchini inahitaji kuwekewa maazingira
ya kukua ili izalishe ajira na mapato ya kodi kwa Serikali. Wakati
Tanzania ndio nchi ya Afrika Mashariki inayoongoza kwa kuwa na Ng’ombe
wengi lakini inaongoza kwa kuagiza maziwa kutoka nje yenye thamani ya
dola za kimarekani 3.6m. Wakati Kenya imelinda soko la Maziwa na Bidhaa
za Maziwa kwa kuondoa (zero rating) kodi ya VAT kwenye bidhaa za Maziwa,
Waziri wa Fedha hajaonyesha kabisa juhudi zozote za kujengea uwezo
sekta ndogo ya Maziwa hapa nchini na hivyo kuweza kuondolewa kabisa
katika ushindani na kujikuta wafugaji wanakosa kabisa soko la kuuza
maziwa yao hapa nchini. Nchi za Rwanda na Uganda pia zimelinda Maziwa na
Bidhaa za maziwa kwa njia hii. Ni muhimu Serikali kuwianisha kodi hii
na Nchi nyingine za Afrika Mashariki.
Mheshimiwa
Spika, Kambi ya Upinzani inapendekeza kufanya marekebisho kwenye sharia
ya Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa kufanya ‘zero rating’ kwenye Maziwa
na Bidhaa za Maziwa zinazozalishwa hapa nchini kwa kipindi cha miaka 5
ili kufikisha uzalishaji wa angalau lita 500,000 za maziwa kwa siku
kutoka lita 123,000 za sasa na kuweza kutoa ajira kwa watanzania zaidi
ya elfu tatu.
Mheshimiwa
Spika, hatua zote za kuongeza mapato tulizopendekeza pamoja na hatua za
Bajeti Mbadala iliyopita ambazo tunarudia kuzipendekeza zitaongeza
Mapato ya Serikali kwa takribani shilingi bilioni 2,885 kama
inavyoonyeshwa katika jedwali hapa chini.
NYONGEZA YA VYANZO VYA MAPATO MBADALA 2012/2013
Chanzo cha Mapato
|
Makisio - Bilioni
|
Marekebisho ya kodi za misitu ikiwemo Mkaa
|
130.8
|
Kupunguza misamaha ya kodi, kuzuia ukwepaji kodi na udanganyifu wa Biashara ya Nje
|
742.74
|
Mauzo ya hisa za serikali
|
415.55
|
Marekebisho ya kodi Sekta ya madini (kodi ya Mapato, Kodi ya CGT na ushuru mbalimbali) (25% ya Mauzo ya Madini Nje)
|
578.36
|
Marekebisho ya Kodi na Usimamizi bora wa Mapato Kampuni za Simu
|
502.26
|
Marekebisho ya Kodi ya SDL
|
243.52
|
Mapato ya wanyamapori
|
61.64
|
Kuondoa msamaha wa ushuru wa mafuta- kampuni za madini
|
44.9
|
Usimamizi wa mapato ya utalii
|
51.75
|
Kuimarisha biashara katika EAC kwa kuongeza mauzo
|
114.15
|
JUMLA
|
2,885.67
|
Mheshimiwa
Spika, kama nilivyosema hapo juu, vyanzo hivi vya mapato ni mjumuisho
wa vyanzo ambavyo katika hotuba zetu mbadala za nyuma tumekuwa
tukipendekeza, ambapo tumevifanyia marekebisho kulingana na hali halisi
ya uchumi ulivyo kwa sasa, pamoja na kupendekeza baadhi ya marekebisho
ya sheria za kodi ili kuongeza mapato zaidi kwa Serikali.
DENI LA TAIFA
Mheshimiwa
Spika, Kambi ya Upinzani inasikitika kwa serikali kuendelea kutengeneza
madeni kwa Taifa kwa kuendelea kukopa zaidi kwa matumizi ya kawaida ya
serikali. Wakati Serikali inasisitiza kwamba Deni letu linastahmilika,
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali anaonyesha mashaka makubwa sana
kutokana na kasi ya kukua kwa Deni la Taifa. Taarifa ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inaonyesha kuwa Deni la Taifa
linazidi kuongezeka kwa asilimia 38 kutoka shilingi trillion 10.5 mwaka
2009/2010 hadi shilingi trillion 14.4 mwaka 2010/2011. Kwa mujibu wa
Waziri wa Fedha Deni la Taifa limefikia shilingi trillion 20.3 mpaka
ilipofika mwezi Machi mwaka 2012. Ukisoma taarifa ya Mwezi wa Mei 2012
ya Benki Kuu ya Tanzania, Deni la Taifa sasa limefikia shilingi trillion
22.
Mheshimiwa
Spika, Suala hapa sio ustahmilivu wa Deni kama inavyodai Serikali bali
ni kwamba tunakopa kufanyia nini? Bajeti ya Mwaka 2012/13
inayopendekezwa inaonyesha kwamba Serikali itakusanya shilingi trilioni
8.7 kama makusanyo ya ndani na itatumia shilingi trilioni 10.6 kama
matumizi ya kawaida. Ni dhahiri kwamba sehemu ya mikopo ambayo serikali
inachukua sasa itakwenda kwenye matumizi ya kawaida. Hatutaki mikopo kwa
ajili ya matumizi ya kawaida ya posho, kusafiri, magari nk. Tuchukue
mikopo kuwekeza kwenye miradi itakayokuza uchumi na kuzalisha kodi
zaidi. Bajeti inaonyesha kwamba Serikali itakopa shilingi takribani
trillion 5 mwaka 2012/13. Serikali ikubali kutekeleza mapendekezo ya
Kambi ya Upinzani ya kuimarisha ukusanyaji wa kodi na kupanua wigo wa
kodi katika maeneo muhimu kama sekta ya madini na mawasiliano, kuzuia
misamaha ya kodi, kutokomeza ukwepaji kodi, na kuepuka matumizi mabaya
ili kuepuka madeni yasiyo ya lazima.
Mheshimiwa
Spika, Kambi ya Upinzani inapenda kusisitiza kwamba Bunge lifanye
ukaguzi maalumu kuhusu akaunti ya Deni la Taifa ili kuweza kubaini
ukweli kuhusu ustahmilivu wa Deni na mikopo ambayo Serikali inachukua
kama inakwenda kwenye Maendeleo na miradi ipi na kama miradi hiyo ina
tija. Vilevile tumependekeza kwamba Mikopo yote ambayo Serikali
inachukua iwe inapata idhini ya Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi au
Bunge litunge sharia ili kiwango cha juu cha kukopa ambacho Serikali
haipaswi kuvuka. Kuiacha Serikali inaendelea kukopa bila mpango ni
kuliweka Taifa rehani na kupeleka mzigo wa kulipa madeni haya kwa kizazi
kijacho. Hatuwezi kukubali Wazee wetu waishi maisha yao, waishi maisha
yetu na pia wakope maisha ya watoto wetu.
Mheshimiwa Spika, Ukiangali
sura ya Bajeti ya Serikali, inaonyesha kuwa Serikali itakopa fedha
zenye masharti ya kibiashara ndani na nje yenye thamani ya Tshs.
Trilioni 2.89 kwa kipindi hiki cha 2012/13. Athari ya mikopo ya
kibiashara ya ndani ni kubwa sana kwa watanzania, kwanza inawafanya
wananchi hasa wajasiriamali wanaokopa kushindana na Serikali yao,
kwani mabenki yatashindwa kuwakopesha wafanyabiashara au wakikopa
watakopa kwa masharti magumu na hasa riba kuwa kubwa. Jambo hili
linapunguza uwezo wa wazalishaji kuongeza uzalishaji hasa viwandani kwa
kukosa mikopo ya uendeshaji. Kama tulivyoshauri hapo juu, Serikali
ijiepushe na mikopo ya masharti ya kibiashara kwa kuongeza makusanyo ya
kodi.
Mheshimiwa
Spika, Kambi ya Upinzani imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya
Serikali kuwa imepata Mshauri Mwelekezi atakayeishauri katika kujiandaa
kufanyiwa tathmini ya uwezo wa kukopa na kulipa madeni. Serikali
ilieleze Bunge ni lini na kwa namna gani zabuni ya kumpata mshauri huyu
ilitangazwa na kama Sheria ya Manunuzi ilifuatwa.
Mwenendo wa Matumizi.
Mheshimiwa
Spika, Serikali inapendekeza Bajeti ya TZS 15 trilioni(USD 8.75
Billion) katika mwaka 2012/13 kama ilivyowasilishwa na Waziri wa Fedha
na Uchumi wiki iliyopita. Uchambuzi wa vitabu vya Bajeti unaonesha
kwamba mafungu ya juu 5 yatakayoongoza kwa matumizi kwenye Bajeti hiyo
ni Kama ifuatavyo;
1. Huduma kwa Deni la Taifa Tshs 2.7 trilioni (USD 1.69 Billion)
2. Wizara ya Ujenzi. Tshs 1 trilioni (USD 625 Million)
3. Wizara ya Ulinzi Tshs 920 bilioni (USD 575 Million)
4. Wizara ya Elimu Tshs 721 bilioni (USD 451 Million)
5. Wizara ya Nishati na Madini Tshs 641 bilioni (USD 400 Million)
Jumla TZS 5.982 Trilioni(USD 3.74 Billlion)
Chanzo: Vitabu vya Bajeti kwa Wabunge
2. Wizara ya Ujenzi. Tshs 1 trilioni (USD 625 Million)
3. Wizara ya Ulinzi Tshs 920 bilioni (USD 575 Million)
4. Wizara ya Elimu Tshs 721 bilioni (USD 451 Million)
5. Wizara ya Nishati na Madini Tshs 641 bilioni (USD 400 Million)
Jumla TZS 5.982 Trilioni(USD 3.74 Billlion)
Chanzo: Vitabu vya Bajeti kwa Wabunge
Mheshimiwa
Spika, Jumla ya mafungu haya ni sawa na asilimia 40% ya Bajeti yote,
kwa hiyo asilimia 40% ya Bajeti yote imepangwa kwa mafungu 5 tu na kati
ya hayo Wizara ni nne tu za Ujenzi, Elimu, Ulinzi na Nishati na Madini.
Wizara ya Kilimo wala Afya hazimo kabisa katika Wizara 5 zitakazopata
fedha nyingi zaidi katika Bajeti. Fungu lenye kiwango kikubwa zaidi ya
Bajeti kuliko vyote ni fungu 22 ambalo ni malipo kwa Deni la Taifa. Pia
sehemu kubwa ya fedha zilizotengwa kwa Ujenzi na Nishati ni madeni kwa
wakandarasi wanaotekeleza miradi ya miaka ya nyuma. Shilingi bilioni 40
ambazo zimetengwa kwa ajili ya Mradi wa Kiwira katika Wizara ya Nishati
na Madini ni kwa ajili ya kulipia Madeni ya Kampuni ya TanPower
Resources ambayo iliuziwa Mgodi wa Kiwira na kushindwa kuundeleza.
Mheshimiwa
Spika, Madhara ya Deni la Taifa yanaonekana hapa katika matuumizi ya
Serikali ambapo tunapokuwa tunalipa madeni tunachukuwa rasilimali fedha
nyingi kutoka kwenye Miradi ya Maendeleo. Wakati Bajeti ya Maendeleo ni
shilingi trilioni 4.5, Bajeti ya kugharamia Deni la Taifa ni shilingi
trilioni 2.7 (sawa na nusu ya Bajeti nzima ya Maendeleo).
Mheshimiwa
Spika, Bajeti ya 2012/13 ni ya kulipa madeni zaidi kuliko Bajeti ya
kuchochea maendeleo ya Taifa letu. Bajeti hii pia yaweza pia kuwa ni
Bajeti ya kukopa zaidi maana jumla ya TZS 5.1 trilioni (USD 3.19 Billion)
zitachukuliwa na Serikali kama mikopo kutoka vyanzo mbalimbali. Mikopo
ya kibiashara ambayo ni mikopo ghali sana itachukuliwa kwa wingi zaidi
kuliko mwaka wa fedha uliopita.
Mheshimiwa
Spika, Mgawanyo wa rasilimali za nchi kwenye sekta za kipaumbele
(Miundombinu ya usafirishaji kama reli, bandari, ndege viwanja vya ndege
n.k), Barabara, nishati,kilimo na mifugo, ili kuinua uchumi zimetengewa
fedha kidogo sana kuweza kuleta tija kulingana na malengo ya Mpango wa
Maendeleo kama ulivyopitishwa na Bunge lako tukufu. Bajeti iliyotengwa
kwa ajili ya nishati imeshuka kwa kiwango cha shilingi 40 bilioni, pia
kwa mwaka uliopita fedha zilizotengwa kwa ajili ya miundombinu,reli na
TEHAMA zilitengwa shilingi 2,781.4 bilioni kwa 2011/12 ikilinganishwa
na shilingi 1,505.1 bilioni kwa mwaka 2010/2011,(hili lilikuwa ni
ongezeko la asilimia 85). Kwa bajeti ya mwaka huu inaonesha sekta
zilezile za vipaumbele; bajeti iliyotengwa ni shilingi 1.394.5 bilion
ambayo ni pungufu ya asilimia 49.86 kwa kulinganisha na mwaka 2011/2013.
Mheshimiwa
Spika, wakati Waziri wa Fedha analiambia Bunge kuwa ametenga shilingi
bilioni 1,383 kwa ajili ya Usafirishaji na Uchukuzi, Wizara ya Ujenzi
imetengewa shilingi bilioni 1,000 kati ya hizo. Wizara ya Uchukuzi yenye
Reli, Bandari, Viwanja vya Ndege na Usafiri wa Maziwa ya Tanganyika,
Nyasa na Viktoria imetengewa chini ya shilingi bilioni 380. Serikali pia
haijasema fedha ambazo zilitengwa na Bunge katika Bajeti inayomaliza
muda wake na kuzielekeza kwenye Wizara ya Miundombinu na Wizara ya
Uchukuzi zimetumikaje maana bado wakandarasi wanadai na fedha za Reli
hazikutoka zote kama ilivyopitishwa na Bunge.
Mheshimiwa
Spika, wizara nyingi hazikupata fedha za Maendeleo kama zilivyopitishwa
na Bunge. Halmashauri za Wilaya ndio zilipata hali mbaya zaidi katika
kupata fedha za Maendeleo ambapo kwa wastani ni asilimia 47 tu ya Bajeti
ndio ilipelekwa katika Halmashauri za Wilaya, Miji na Manispaa.
Kutokana na hali hii Wabunge kama wawakilishi wa wananchi walihoji
Serikali kwenye Kamati zao na kupata majibu ambayo sio ya kuridhisha
hivyo kupelekea Wabunge kugomea baadhi ya Wizara.
Mheshimiwa
Spika, Ushahidi wa hayo ni baadhi ya Kamati za Kudumu za Bunge kukataa
kukubali Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa baadhi ya Wizara zilizo
chini ya Kamati hizo. Wizara ambazo hazikupitishiwa /Kukubaliwa
makadirio yake ni pamoja na;
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi,
Wizara
ya Uchukuzi, na (nilishangaa kumwona Waziri wa Uchukuzi akiwaahidi
wananchi pale Jangwani kwamba Reli inakarabatiwa vya kutosha ilhali
Kamati haijapitisha Makadirio ya Matumizi ya Wizara yake kwa kuwa
haikupewa fedha za kutosha)
Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika
Mheshimiwa
Spika, kabla Bunge lako tukufu halijajadili Makadirio ya Matumizi ya
mwaka unaokuja ni vema Serikali itueleze kwanza fedha zilizotengwa mwaka
uliopita na hazikufika hatima yake nini?
Mheshimiwa
Spika, uwiano wa bajeti iliyotengwa kwa matumizi ya kawaida ambayo ni
asilimia 70% wakati bajeti ya maendeleo asilimia 30% haiwezeshi nchi
kupiga hatua ya haraka ya Maendeleo. Kama ilivyoonyeshwa na Waziri
Kivuli Mipango na nitakavyohitimisha hotuba hii, Serikali imetayarisha
Bajeti hii bila kuzingatia masharti yaliyowekwa na Mpango wa Maendeleo
uliopitishwa na Bunge kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu ibara ya 63
(3)(c) kwa kutotenga asilimia 35 ya Mapato ya ndani ya Serikali kwenye
Bajeti ya Maendeleo.
Mheshimiwa
Spika, Serikali imekuwa ikitenga fedha kidogo katika miradi ya
maendeleo katika bajeti zake. Kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), matumizi ya kawaida ya
Serikali yanaongezeka huku matumizi katika shughuli za maendeleo
yanapungua mwaka hadi mwaka. Takwimu katika jedwali hapa chini
zinaonyesha
Fungu
|
2009/2010
|
%
|
2010/2011
|
%
|
Fedha za matumizi ya kawaida (Sh)
|
6,251,629,581,428
|
73
|
7,587,424,923,903
|
77
|
Fedha za matumizi ya maendeleo (Sh)
|
2,299,010,652,135
|
27
|
2,223,684,150,465
|
23
|
Jumla
|
8,550,640,233,563
|
100
|
9,811,109,074,368
|
100
|
Chanzo: Ripoti ya CAG, uk. 21
Aidha,
kwa miaka miwili iliyopita yaani 2009/2010 na 2010/2011 kumekuwa hakuna
uwiano wa fedha za Maendeleo kama bajeti zilivyopitishwa na Bunge dhidi
ya fedha zinazotolewa na hazina kwa ajili ya maendeleo katika Wizara na
Idara. Tazama jedwali;
Mwaka
|
Bajeti iliyoidhinishwa
|
Fedha halisi zilizotolewa
|
Tofauti (Sh)
|
%
|
2009/2010
|
2,825,431,400,000
|
2,299,010,652,135
|
526,420,747,865
|
19
|
2010/2011
|
3,750,684,569,000
|
2,223,684,150,465
|
1,527,000,418,535
|
41
|
Chanzo: Ripoti ya CAG, uk.22
Mheshimiwa
Spika, Kutokana na takwimu hizi, jumla ya Sh. 1,527,000,418,535 au
asilimia 41 ya fedha zilizoidhinishwa kwa maendeleo hazikutolewa katika
mwaka wa fedha 2010/2011, na kiasi cha Sh. 526,420,747,865 au asilimia
19 ya fedha zilizoidhinishwa mwaka 2009/2010 hazikutolewa pia. Hii ina
maana kuwa shughuli za maendeleo za kiasi hicho cha fedha
hazikutekelezwa kwa miaka husika.
Mheshimiwa
Spika, Kambi ya Upinzani inatafsiri hali hiyo kama utovu mkubwa wa
nidhamu ya matumizi ya fedha za umma kwa upande wa Serikali, Vilivile
inaonesha ni jinsi gani Serikali yetu haithamini maendeleo ndio maana
kila mwaka Serikali inazidisha matumizi yake na kuhakikisha kuwa
inayapata kwa wakati huku ikipunguza bajeti ya maendeleo na kutotoa
fedha zote kama zilivyoidhinishwa na mbaya zaidi hata zile zinazotolewa
hazitolewi kwa wakati muafaka. Hii inafanya kukaa hapa Dodoma na
kupitisha Bajeti kuwe hakuna maana maana Bajeti haitekelezwi kama
ilivyopitishwa.
Mheshimiwa
Spika, Kiasi kinachotengwa kwa ajili ya maendeleo kimeshuka kutoka
shilingi trilioni 4.9 katika mwaka wa fedha 2011/12 hadi kufikia kiasi
cha shilingi trililioni 4.5 mwaka huu wa fedha 2012/13. Pamoja na
serikali kushindwa kutekeleza miradi ya maendeleo katika bajeti
iliyopita, bado imeendelea kupunguza bajeti ya maendeleo katika bajeti
hii. Ni dhahiri serikali haizingatii swala la maendeleo ya mwananchi,
pia kutoona njia ya kuweka mkazo katika maendeleo na kuendelea kupuuzia
maazimio ya mpango wa maendeleo wa miaka mitano.
Mheshimiwa
Spika, katika Bajeti mbadala, Kambi ya Upinzani imetenga asilimia 36.06
na kukidhi matakwa ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa kutoka katika mapato
ya ndani kwa matumizi ya maendeleo kama Mpango wa Maendeleo ya Taifa
ulivyoelekeza.
Mheshimiwa
Spika, Tuliamua kama Taifa kwamba Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano
ndio safina yetu ya kuelekea nchi ya ahadi (middle income country).
Mpango ukapitishwa na Bunge na kuwekwa sahihi na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Inasikitisha kuona kuwa Serikali inatoboa kisiri
siri safina hii wakati tupo kati kati ya maji! Ninaamini wananchi
wanawaona wanaotoboa safina yetu na watawatosa kabla hawajazamisha Taifa
zima kwa kushindwa kutekeleza Mpango unavyoelekeza.
Ubadhirifu wa fedha zinazotengwa
Mheshimiwa
Spika, pamoja na fedha za maendeleo kutolewa kidogo kulinganisha na
bajeti inayopitishwa na Bunge, bado kumekuwepo na matumizi yasiyo na
tija na ubadhirifu mkubwa.
Mheshimiwa Spika, upotevu wa fedha za umma umeendelea kuwa kikwazo
kikubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi. Uchambuzi wetu juu ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2010/2011 pekee, umebaini takribani jumla ya Bilioni 12.9 (12,968,168,985) za fedha za umma zimepotea kama ongezeko kutoka shilingi billion 11.9 (11,152,048,065) ambazo ni sawa na ongezeko la asilimia 14 ya upotevu wa fedha za Serikali kwa mwaka wa fedha 2009/2010,hii inaonyesha kuwa Serikali inaona ni jambo la kawaida kupoteza viwango hivi vya pesa za Serikali na kambi ya upinzani kuwasisistiza wananchi kuendelea kuitathmini Serikali yao sasa ili kuweza kufanya maamuzi sahihi dhidi ya Serikali yao.
kikubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi. Uchambuzi wetu juu ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2010/2011 pekee, umebaini takribani jumla ya Bilioni 12.9 (12,968,168,985) za fedha za umma zimepotea kama ongezeko kutoka shilingi billion 11.9 (11,152,048,065) ambazo ni sawa na ongezeko la asilimia 14 ya upotevu wa fedha za Serikali kwa mwaka wa fedha 2009/2010,hii inaonyesha kuwa Serikali inaona ni jambo la kawaida kupoteza viwango hivi vya pesa za Serikali na kambi ya upinzani kuwasisistiza wananchi kuendelea kuitathmini Serikali yao sasa ili kuweza kufanya maamuzi sahihi dhidi ya Serikali yao.
MAPENDEKEZO YA KAMBI YA UPINZANI
SERA YA MATUMIZI 2012/13 KWA BAJETI MBADALA
Mheshimiwa
Spika, lengo kuu la Bajeti Mbadala ni kuhakikisha uchumi unakua katika
maeneo ya vijijini kwa kati ya asilimia 6 na 8 ili kuleta Maendeleo ya
wananchi na kutokomeza umasikini. Kwa njia hiyo ni dhahiri wananchi
wapatao milioni 30 waishio vijijini watanufaika na matumizi ya raslimali
zao.
Vipaumbele vya bajeti ya Matumizi.
Kujenga
Mazingira ya Ukuaji wa uchumi vijijini (rural growth) kwa kuboresha
miundombinu ya umeme, barabara, maji na miundombinu ya Umwagiliaji.
Tunapendekeza kutumia shilingi bilioni 600 kila mwaka (bilioni 150 kwa
kila sekta niliyotaja). Fedha hizi zitasimamiwa na Mamlaka ya Maendeleo
Vijijini (Rural Development Authority – to be established) itakayokuwa
chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Kukarabati
Reli ya Kati na matawi yake ya Tanga/Arusha na Mpanda. Tutatenga tshs
443bn kwa RAHCO kwa ajili ya Reli. Lengo ni kuhakikisha Reli ya Kati
inafikia uwezo wa kusafirisha Tani 1.5m kwa mwaka na hivyo kulipatia
Taifa fedha za kigeni katika sekta ya usafirishaji kupitia Bandari ya
Dar es Salaam. Tunataka sekta ya usafirishaji iliingizie Taifa fedha za
kigeni mpaka dola za kimarekani 1.5 bilioni kutoka dola 0.5 bilioni za
sasa.
Kuboresha
Elimu na Afya hasa kwa Shule na Zahanati/Vituo vya Afya vya Vijijini
kwa kutoa motisha kwa wafanyakazi wa Sekta hizi walio kwenye Halmashauri
za Wilaya. Tunapendekeza posho za Mazingira ya Vijijini kwa Walimu,
Madaktari na Manesi sawa na mara moja na nusu ya Mishahara yao. Vile
vile tutaongeza mishahara ya Walimu, Manesi na Madaktari kwa asilimia
50, pamoja na kuboresha stahili zingine za kazi ili kuvutia Watanzania
wengi zaidi katika maeneo haya na kuboresha huduma zao kwa wananchi.
Kuongeza Kima cha chini cha Mshahara kwa Wafanyakazi wa Umma mpaka Tshs 315,000 kwa Mwezi
Kuanzisha Pensheni ya uzeeni kwa Wazee wote nchini wenye umri wa zaidi ya miaka 60.
Kujenga
Uwezo wa Viwanda vya ndani ili Kuuza nje bidhaa za kilimo na mifugo
zilizoongezewa thamani. Tutazuia kuuza nje Korosho ghafi na Ngozi ghafi
kwa kuanzia. Lengo ni kufufua viwanda vyote vya nguo na kuanzisha
viwanda vipya kwa kutoa motisha kwa wawekezaji watakaotumia malighafi za
hapa nchini.
Kupunguza
mzigo wa matumizi ya magari ya Serikali kwa kupiga mnada baadhi ya
‘mashangingi’ na kuweka mfumo wa kukopesha Magari kwa watumishi wote wa
Umma wanaostahili Magari kama alivyofanya Gavana wa Benki Kuu ya
Tanzania. Katika Taarifa yake kwa Kamati ya Fedha na Uchumi, Waziri wa
Fedha alitamka, ‘….kufanya mapitio ya stahili za aina za magari kwa
viongozi wa ngazi mbalimbali na kuandaa mwongozo wa kugharamia ununuzi
wa vyombo vya usafiri ili kupunguza matumizi ya magari, mafuta na
matengenezo ya magari…’ kama hatua za kubana matumizi. Hatua hii ya
kupunguza gharama za magari Waziri hakuisema kabisa katika hotuba yake
Bungeni.
Kuendelea
kusisitiza kufutwa kwa posho za vikao katika mfumo mzima wa malipo na
stahili kwa watumishi wa Umma. Katika Taarifa yake kwa Kamati ya Fedha,
Waziri wa Fedha alitamka ‘…. Kufanya mapitio ya posho na stahili zote
kwa lengo la kuziwianisha….’ Suala hili nalo Waziri hakulizungumza
kabisa katika Hotuba yake Bungeni.
Kuanzisha
Chuo Kikuu cha Mtwara (Mtwara University for Petroleum Studies) ili
kuzalisha wataalamu wa kutosha wa Sekta ya Mafuta na Gesi na kuliandaa
Taifa kuwa na wasomi mahiri wa maeneo hayo na hivyo kufaidika na Utajiri
wa Mafuta na Gesi uliopo nchini kwetu. Tunapendekeza shilingi bilioni
200 mwaka huu katika Bajeti ya Wizara ya Elimu kwa ajiri ya Mradi huu.
Kutunga
sheria mpya ya Mashirika ya Umma (Public Corporations Act) ili kujengea
uwezo Ofisi ya Msajili wa Hazina ili kusimamia vyema Mashirika yote ya
Umma ambayo Serikali inamiliki kwa zaidi ya asilimia 100 na kutoa nguvu
za kisheria kwa Shirika la CHC kuweza kusimamia hisa za Serikali katika
Kampuni na Mashirika ambayo Serikali inamiliki chini ya asilimia 50.
Kupunguza
gharama za safari za nje kwa kupunguza ukubwa wa misafara na madaraja
ya kusafiria. Eneo hili la safari za nje limekuwa likiigharimu Serikali
fedha nyingi sana.
Mheshimiwa
Spika, kufuatia hatua mbali mbali za kikodi tulizozichukua Kambi ya
Upinzani inapendekeza Bajeti ya shilingi trilioni 15 ambazo zitapatikana
kwa Mapato ya ndani ya shilingi trilioni 11.9 na misaada na mikopo ya
kibajeti ya shilingi trilioni 3.2 kama ilivyopendekezwa na Serikali.
Kambi ya Upinzani inapendekeza Serikali kutokukopa kibiashara ili
kudhibiti ukuaji wa Deni la Taifa.
Mheshimiwa
Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kwamba Serikali itatumia
shilingi trilioni 9 katika Matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 6
kama Matumizi ya Maendeleo. Katika fedha za Maendeleo, asilimia 35 ya
Mapato ya ndani yameelekezwa huko kama ilivyoagizwa na Mpango wa
Maendeleo ya Taifa ulioidhinishwa na Bunge kwa mujibu wa Katiba.
SURA YA BAJETI MBADALA YA MWAKA 2012/2013
MAPATO
|
SHILINGI MILIONI
| ||
A
|
Mapato ya ndani
|
11,889,078
| |
i)mapato ya kodi (TRA)
| |||
ii)Mapato yasiyo ya kodi
| |||
B
|
Mapato ya Halmashauri
| ||
C
|
Mikopo na Misaada ya kibajeti (GBS)
|
842,487
| |
D
|
Misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo nay a kisekta
|
2,314,231
| |
i)Misaada
|
1,465,461
| ||
ii)Misaada na mikopo kisekta
|
415,137
| ||
iii)MCC(MCA-T)
|
433,634
| ||
Jumla ya Misaada na mikopo ya kibajeti
|
3,156,718
| ||
JUMLA YA MAPATO YOTE.
|
15,045,796
| ||
MATUMIZI
| |||
E
|
Matumizi ya Kawaida
|
9,000,000
| |
H
|
Matumizi ya Maendeleo
| ||
(i)Fedha za ndani
|
4,161,177
| ||
(ii)Fedha za Nje
|
1,884,619
| ||
Jumla ya matumizi ya maendeleo
|
6,045,796
| ||
JUMLA YA MATUMIZI YOTE.
|
15,045,796
|
Hitimisho
Fedha za Rada
Mheshimiwa
Spika, Wakati Kamati za Bunge zilipokaa kujadili taarifa ya Serikali
kuhusu Mfumo wa Mapato na Matumizi, Waziri wa Fedha na Uchumi alitoa
Taarifa kuhusu Fedha za Rada zilizorejeshwa, jumla ya shilingi 72.3
bilioni ambazo zilipokelewa tarehe 26 Machi, 2012. Kwa mshtuko wa
Wabunge, Waziri aliiambia Kamati kuwa mchakato wa manunuzi ya vitabu na
madawati kwa kutumia fedha hizi ulikuwa umeanza chini ya Ofisi ya Waziri
Mkuu TAMISEMI. Fedha hizi hazijawahi kupitishwa na Bunge lako tukufu.
Kitendo cha Serikali kuzitumia kabla ya kupitishwa na Bunge ni kuvunja
sheria za Fedha kuhusiana na masuala ya Bajeti. Wakati Waziri
akiwasilisha Hotuba yake hakugusia kabisa suala la fedha zilizorejeshwa
kutokana na Ununuzi wa Rada!
Mheshimiwa
Spika, Kambi ya upinzani inataka maelezo ya Serikali juu ya Fedha hizi
na utaratibu wa kuzitumia. Kambi inataka kufahamu vigezo vilivyotumika
kuteua mikoa ya Mwanza, Morogoro na Dar es Salaam kutumia fedha hizi.
Kambi pia inapenda kufahamu Deni lililochukuliwa kununua Rada hii
iliyoleta kashfa kubwa sana hapa nchini limefikia kiasi gani kulilipa na
tukililipa tutakuwa tumelipa kiasi gani kwa ujumla.
Mheshimiwa
Spika, Uumbaji wa bajeti ya Serikali umekuwa ni ule ambao unapendelewa
zaidi na wale wavivu wa kufikiri, yaani mfumo rahisi, wataalamu wanauita
Incremental Budgeting. Mfumo huu hujikita zaidi katika kutizama
ukuaji wa mapato na kugawa mapato hayo kwa mtindo wa nyongeza ya
asilimia Fulani toka katika bajeti iliyotangulia. Mfumo huu huacha
kuzingatia mambo mengi mtambuka. Mfano, tunaweza tizama sekta mojawapo
ya umeme ambapo tukifanya uumbaji wa bajeti kwa mfumo wa kiasi cha
nyongeza (incremental budget) kuna thamani halisi ambazo ukizitizama kwa
bei wazi ya soko tayari zimepaa sana ndani ya miezi kumi na miwili.
Mheshimiwa
Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni, tukiwa ni serikali ambayo tunasubiri
kukabidhiwa dola, tunapendekeza kwamba ni vema tukaanza kutizama
uwezekano wa matumizi ya Zero Budgeting ambapo japo ni mfumo
ambao unahitaji kazi ya ziada, lakini una faida sana kwani hutizama
mipango ya matumizi kulingana na wakati uliopo huku ikifanya rejea ya
wakati uliopita.
Mheshimiwa
Spika, Kambi ya Upinzani pia inapendekeza kwamba Bajeti za Mashirika ya
Umma ziwe sehemu ya Bajeti Kuu ya Nchi kwani kuna masuala mengi
yanayotekelezwa na Mashirika haya na Wananchi kupitia Bunge hawayajui.
Ni vema katika mfumo mpya wa Bajeti tutakaokuwa nao kufuatia mapendekezo
ya Spika wa Bunge ambapo kutakuwa na Ofisi ya Bajeti ya Bunge na Kamati
ya Bunge ya Bajeti, Sheria ya Bajeti (Fiscal Responsibility Act/Budget
Act) izingatie suala la kuziweka kama viambatisho Bajeti za Mashirika ya
Umma katika Bajeti ya Nchi.
Mheshimiwa
Spika, Bajeti ya Serikali ya mwaka huu kama ilivyowasilishwa na Waziri
wa Fedha imewasahau kabisa wananchi wa vijijini na haina mkakati wowote
wa kuwakomboa watanzania walio wengi wanaoishi huko. Mipango mingi ya
kikodi katika sera ya Mapato ya Serikali itasaidia wakazi wa mijini
ambao ni asilimia 25 tu ya Watanzania wote.
Mheshimiwa
Spika, Kambi ya upinzani inapenda kuweka msisitizo kwamba Tanzania bado
ni nchi ya Wakulima maana robo tatu ya Watanzania wanaishi vijijini
ambapo hawajui hizi hadithi za Uchumi kukua tunazoimba na kupewa sifa
kila siku. Hawa ni watu milioni 30 ambao hawana Maji, hawana Umeme,
mazao yao hayafiki sokoni maana hawana barabara nzuri, shule wanazosoma
watoto wao hazina walimu maana wanakimbia mazingira magumu. Hawa
Watanzania wa chini milioni 30 (The Bottom 30M) tunaowawakilisha hawana
bima mazao yakiharibiwa na wala hawana pensheni wanapokuwa wamezeeka na
kupoteza nguvu za kufanya kazi. Hawa ‘The Bottom 30M’ bado wanaishi
maisha walioshi babu zetu. Hawa Watanzania milioni 30 tumewasahau.
Tunajenga Mataifa mawili ndani ya nchi moja, moja la mafukara
(wanavijiji) na moja la wanaojiweza (wamijini).
Mheshimiwa
Spika, Kama tunataka kujibu kitendawili cha kuwa na Uchumi unaokua kwa
kasi lakini haupunguzi umasikini inabidi kuelekeza nguvu zetu vijijini
walipo Watanzania wengi. Kukuza Uchumi wa Vijijini kwa kuwekeza kwenye
misingi ya kujenga uchumi imara ndio njia pekee ya kutokomeza ufukara wa
Watanzania.
Mheshimiwa
Spika, Bajeti Mbadala ya Kambi ya Upinzani mwaka huu ni Bajeti ya
Ukombozi wa mwananchi. Licha ya kwamba tunahitaji ukuaji wa kasi zaidi
wa uchumi. Changamoto sasa ni namna gani ukuaji huu wa uchumi unawafikia
wananchi milioni thelathini wa Vijijini na kuboresha maisha yao.
Mheshimiwa
Spika, KWA KUWA Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano uliwasilishwa
Bungeni na Serikali na kupata pongezi nyingi sana kutoka kwa waheshimiwa
wabunge lakini cha kushangaza Serikali hii ya Chama Cha Mapinduzi
imeshindwa kuutekeleza kwa vitendo mpango huu wa Taifa. Mwaka wa kwanza
Mpango haukuwekewa fedha kwa kuwa ulikuwa wa Mpito. Mpango unahitaji
angalau shilingi trillion Nane kila mwaka ili uweze kutekelezwa. Mpango
ulipata shilingi trillion moja tu mwaka 2011/12.
Mheshimiwa
Spika, KWA KUWA Bunge liliazimia namna ya kuhakikisha tunapata fedha za
kuendeleza nchi yetu sisi wenyewe, naomba kunukuu ukurasa wa 92 kifungu
cha 4.3.1 katika Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano toleo la kiswahili
kama ifuatavyo ‘kwa kuelewa kuwa wakati wote kutakuwa na miradi ya
uwekezaji nje ya mpango, serikali, kuanzia sasa, itakuwa inatenga
asilimia 35 ya makadirio ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kugharamia
bajeti ya maendeleo kila mwaka’ mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa
Spika, KWA KUWA katika makadirio ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa
Fedha 2012/13 Serikali imetenga asilimia sifuri ya Mapato ya ndani kwa
ajili ya kugharamia Bajeti ya Maendeleo. Serikali hii imeshindwa
kusimamia ahadi zake yenyewe kama inavyoonekana katika mpango wa
maendeleo ya miaka mitano. Serikali hii ya CCM imeshindwa kuheshimu
Uamuzi uliopitishwa na Bunge kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania ya mwaka 1977.
Mheshimiwa
Spika, KWA KUWA Kwa mujibu wa ibara ya 63(3)(c ) madaraka ya Bunge ni
pamoja na ‘Kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu au wa
muda mfupi unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano, na
kutunga sheria ya kusimamia utekelezaji wa mpango huo”. Bunge
liliidhinisha Mpango kwa mujibu wa ibara tajwa ya Katiba.
Mheshimiwa
Spika, KWA KUWA Bajeti ya mwaka 2012/13 iliyowasilishwa Bungeni na
Waziri wa Fedha na Uchumi haikukidhi matakwa ya Mpango wa Maendeleo kama
ambavyo ulipitishwa na Bunge, HIVYO BASI,
Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali iiondoe (withdraw) Bungeni Bajeti
iliyoileta ili ikatayarishwe upya ili ikidhi matakwa (compliance) ya
Mpango wa Maendeleo kama ulivyoidhinishwa na Bunge na kusainiwa na Rais
wa nchi.
Mheshimiwa Spika Naomba Kuwasilisha
………………………………………………….
Kabwe Zuberi Zitto, Mb
Waziri wa Fedha na Uchumi Kivuli
18.06.2012
SURA YA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2012/2013.
MAPATO
|
%
|
SHILINGI MILIONI
| ||
A
|
Mapato ya ndani
|
57.63
|
8,714,671
| |
i)mapato ya kodi (TRA)
|
8,070,088
| |||
ii)Mapato yasiyo ya kodi
|
644,583
| |||
B
|
Mapato ya Halmashauri
|
362,206
| ||
C
|
Mikopo na Misaada ya kibajeti (GBS)
|
5.57
|
842,487
| |
D
|
Mikopo na misaada ya miradi ya maendeleo na ya kisekta
|
15.30
|
2,314,231
| |
E
|
Mikopo ya ndani
|
10.78
|
1,631,231
| |
F
|
Mikopo yenye masharti ya kibiashara
|
8.25
|
1,254,092
| |
JUMLA YA MAPATO YOTE.
|
15,119,644
| |||
MATUMIZI
| ||||
E
|
Matumizi ya Kawaida
|
71.06
|
10,591,805
| |
Deni la taifa
|
2,745,056
| |||
Mishahara
|
3,781,100
| |||
Matumizi Mengineyo
|
4,065,649
| |||
Wizara
|
3,311,399
| |||
Mikoa
|
49,701
| |||
Halmashauri
|
704,549
| |||
H
|
Matumizi ya Maendeleo
| |||
(i)Fedha za ndani
|
2,231,608
| |||
(ii)Fedha za Nje
|
2,34,231
| |||
Jumla ya matumizi ya maendeleo
|
29.94
|
4,527,839
| ||
JUMLA YA MATUMIZI YOTE.
|
TOFAUTI KATI YA BAJETI YA SERIKALI NA BAJETI MBADALA YA KAMBI RASMI YA UPINZANI
Bajeti Mbadala ya Kambi ya Upinzani2012/2013
|
Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2012/2013
|
Kukuza uchumi vijijini.
|
Mwelekeo na malengo ya Serikali hauleweki, hatua zilizochukuliwa ni koboresha uchumi wa mijini.
|
Njia mbadala zinazotekelezeka za kupunguza mfumuko wa bei.
|
Kuwa na njia zilezile zilizoshindwa mwaka wa fedha uliopita za kupunguza mfumuko wa bei.
|
Kunufaika
na mapato ya mitaji “Capital gains” kwa kutoza kodi kwa mali za
kampuni zilizopo nchini kwa mauzo yanayofanyika nje ya nchi na hivyo
kupanua wigo wa TRA kutoza kodi
|
Kutoza hisa kwa mauziano ya hisa pekee kwa mauziano yanayofanyika nje. Hisa inapunguza wigo wa TRA kutoza kodi.
|
Kupanua
wigo wa kodi ya tozo la ujuzi (SDL)kwa kuijumuisha serikali na
mashirika ya umma na kupunguza mzigo kwa sekta binafsi pekee.
|
Kupitia upya SDL bila kuonyesha namna itakavyofanyika.
|
Kupunguza misamaha ya kodi kutoka 3% ya sasa hadi 1% ya pato la taifa.
|
Kurudia ahadi zilezile za mwaka jana za kupitia upya misamaha ya kodi bila kuleta mrejesho wa kile walichokifanya.
|
Kuboresha kodi sekta ya madini ili kupelekea taifa kupata nagalau 25% ya mazuo ya madini nje kama mapato ya serikali.
|
Kutokuwa na hatua yoyote ya kuongeza mapato ya Serikali kutoka katika sekta ya madini.
|
Kulipa kima cha chini cha mshahara kuanzia shilingi 315,000.
|
Kulipa shilingi 170,000 kama kima cha chini.
|
Kulipa pensheni kwa wazee wote kuanzia miaka 60 na kuendelea
|
Kutokuwa na mfumo wa pensheni kwa wote.
|
Kushusha
kiwango cha chini kodi ya mapato kwa wafanyakazi (PAYE) kutoka 14%
hadi 9% ili kumpunguzia mfanyakazi makali ya maisha na kutoza kodi
zaidi kwa watu wenye kipato kikubwa
|
Kubaki
na kiwango kilekile cha chini cha kodi ya 14% na kubakiza mfumo ule
ule wa kodi ya Mapato unaomfanya Masikini alipe zaidi ya Tajiri.
|
Kuziba mianya kwa makampuni ya simu kukwepa kutokulipa kodi ya mapato.
|
Kuongeza ushuru wa bidhaa kwenye muda wa maongezi na hivyo kumwongezea gharama mwananchi.
|
Kuondoa mikopo ya kibiashara ili kulipunguzia taifa mzigo wa madeni
|
Kuendelea mikopo na hivyo kuongeza deni la taifa. mingi ya kibiashara.
|
Kutenga
asilimia 35 ya mapato ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya
maendeleo kama ilivyoelekezwa kwenye mpango wa maendeleo wa miaka
mitano.
|
Kutenga
asilimia sifuri ya fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya miradi ya
maendeleo na hvyo kutokutekeleza mpango wa taifa .
|
Utegemezi wa Bajeti 21.3%
|
Utegemezi wa Bajeti 42.37%
|
JEDWALI LA ULINGANISHO WA ASILIMIA KWA BAJTEI MBILI
UPINZANI
|
ASILIMIA
|
SERIKALI
|
ASILIMIA
| |
Mapato ya ndani
|
78.70
|
Mapato ya ndani
|
57.63
| |
Mikopo na Misaada ya kibajeti (GBS)
|
5.57
|
Mikopo na Misaada ya kibajeti (GBS)
|
5.57
| |
Misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo na y a
kisekta
|
15.30
|
Misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo na y a
Kisekta
|
15.30
| |
Mikopo ya masharti ya kibiashara ya ndani
|
0
|
Mikopo ya masharti ya kibiashara ya ndani
|
10.78
| |
Mikopo ya masharti ya kibiashara ya nje.
|
0
|
Mikopo ya masharti ya kibiashara ya nje.
|
8.25
| |
Matumizi ya Kawaida
|
59.22
|
Matumizi ya Kawaida
|
71.06
| |
Matumizi ya Maendeleo
|
40.78
|
Matumizi ya Maendeleo
|
29.94
| |
Matumizi ya maendeleo fedha za mapato ya ndani
|
36.06
|
Matumizi ya maendeleo fedha za ndani
|
0
| |
Matumizi ya maendeleo fedha za nje
|
12.39
|
Matumizi ya maendeleo fedha za nje
|
29.94
|
0 comments:
Post a Comment