Searching...
Wednesday, September 14, 2011

Neno La Leo; Mwanadamu Anakuwaje Anapokumbwa Na Maafa?



Ndugu zangu,
NCHI yetu imekumbwa na msiba mkubwa, ni maafa.  Ni ajali ya meli ya MV. Spice Islanders iliyotokea juma la jana kule pwani ya Nungwi, Zanzibar.

Na swali ni je; mwanadamu anakuwaje anapokumbwa na maafa?
Jibu; kwanza kabisa, maafa yana nadharia yake pindi  yanapotokea. Maafa yeyote yale  yana hatua  mbili kubwa;  mosi, mshtuko mkubwa kwa mwanadamu pindi maafa yanapomtokea, na pili, kwa mwanadamu  kufanyia kazi kilichotokea.

Tumeona, kuwa Watanzania tulipatwa na mshtuko mkubwa  tulipofikiwa na taarifa za maafa ya meli kuzama  kule Zanzibar.  Hatua ya sisi wanadamu kukumbwa na hali ya mshtuko mkubwa pindi maafa yanapotokea  hutuchukua saa kadhaa hadi siku kadhaa kabla ya hali hiyo kuanza kuondoka taratibu.

Ni katika hali hii ya kwanza ya mshtuko mkubwa, mwanadamu mwenzetu aliyekumbwa na maafa huonekana kutoamini kilichotokea kwamba kimetokea. Anaweza hata kucheka ndani ya mzigo mkubwa wa huzuni ulio katika nafsi yake.

Kuna ambao hubaki kudhani ni ndoto tu. Ni wakati huu pia sisi wanadamu hupatwa na hasira, chuki na ghadhabu  kwa kilichotokea. Na hata baada ya kutamka ya ghadhabu, huzuni uturejea tena kama wingu zito la mvua linalotanda kwa kasi. Ni hapa wanadamu tunapojihisi ni wenye mkosi.

Tunajiona tusio na uwezo wa kufanya lolote kurekebisha hali husika. Tunajikuta katika hali ya ombwe kuu. Tunahisi  tumo katika giza nene. Tunaishiwa nguvu. Tunajiuliza  maswali mengi. Hatuyapati majibu tukaridhika. Ni katika hali hii, kila mkono wa pole tunaopewa na mwanadamu mwenzetu unakuwa na maana kubwa sana.

Hata ’ missed calls’ kwenye simu unazihesabu kuwa ni ’ missed calls’ za kukutia faraja. Kwamba kuna wanadamu wenzako wenye kukujali. Ndio, maafa huwaunganisha wanadamu. Na kuna maadui wanaopatana kwenye maafa. Maana, ndipo hapo hutambua, kuwa siku zote, wanadamu tunahitajiana. Ndio maana tukaitwa wanadamu, na si wanyama.

Baada ya hatua hiyo ya kwanza ya maafa yanapotokea, huja hatua ya pili, nayo ni ya kufanyia kazi kilichotokea. Hapa wanadamu, katika hali ya kutulia,  tunaanza kuirejea ile hali ya maafa iliyotumbuka na kujaribu kuielewa.  

 Tunatafuta tafsiri na maana ya kilichotokea.  Ni hapa , ndipo  wanadamu tunaanza kuelewa,  kuwa kilichotokea kimetokea. Katika hatua hii tunahitaji zaidi kuzungumza kwa sauti  juu ya kilichotokea. Na katika kufahamu ni  kitu gani kingefanyika ili kukizuia kilichotokea.

Na yote haya ni  katika hitaji letu  wanadamu la kutaka  kuutafuta ukweli na kujifunza. Tuutafute ukweli  ili siku nyingine kisije kutokea tena kile kilichotokea. Hapa wanadamu  tunaanza kurejea katika hali ya kawaida.  Kwa kawaida, hatua hizi mbili hutuchukua wanadamu majuma takribani sita kuzipitia na kuzimaliza.

Kinachohitajika hapa ni kwa wanadamu wengine kuelewa hitaji la mwanadamu mwenzao kuzipitia hatua hizi. Na si baada ya juma moja tu kudhani kuwa mwanadamu aliyekumbwa na maafa  na huzuni ya msiba mkubwa anaweza kurejea katika hali ya kawaida.

Kikubwa ni  kuzungumza kwa uhuru juu ya kilichotokea kwa nia njema ya kutaka kujifunza na kuepuka hali hiyo isitokee tena. Maana,  Watanzania tumekuwa ni watu wa kumwachia Mungu kwa hata yale tunayopaswa kuyafanya wenyewe.

Na labda nimalizie kwa kuuliza; hivi  tumejiandaa vipi kama  jiji kama Dar es Salaam  linakumbwa na maafa ya mafuriko makubwa? Au maafa ya gesi kulipuka? 
Nahitimisha Neno La Leo. ( Neno hili ni sehemu ya makala yangu iliyochapwa leo kwenye Raia Mwema)

Na Maggid,
Dar Es Salaam.
Septemba 14, 2011

0 comments:

WELCOME URARY95 SPORTS NEWS BLOG | ADVERTISE YOUR BUSINESS HERE AT A CHEAP PRICE MORE INFORMATION CONTACT US: 0654315901 | Email: urary95@yahoo.com | KARIBU URARY95 SPORTS NEWS BLOG | TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA GHARAMA NAFUU KWA MAELEZO ZAIDI WASILIANA NASI: 0654315901 | Barua Pepe: urary95@yahoo.com
 
Back to top!