Searching...
Saturday, May 21, 2011

Sheikh Yahya Hussein afariki dunia

Sheikh Yahya Hussein
Mnajimu maarufu wa Afrika Mashariki, Sheikh Yahya Hussein amefariki dunia nyumbani kwake jijini Dar es Salaam, Tanzania kutokana na maradhi ya moyo.
Sheikh Yahya ambaye wakati wa uhai wake alipata umaarufu mkubwa kutokana na kutabiri matukio makubwa katika maeneo mbalimbali duniani, alizaliwa wilaya ya Bagamoyo mkoa wa Pwani, mashariki mwa Tanzania mwaka 1932.
Alipata elimu yake ya awali katika shule ya Al Hassanain jijini Dar es Salaam, kabla ya kwenda visiwani Zanzibar ambako aliendelea na masomo katika chuo cha Muslim Academy.
Baada ya kuhitimu alikwenda nchini Misri alikopata elimu ya juu zaidi katika masuala ya dini ya Kiislam katika chuo kikuu cha Al Azhar kilichoko jijini Cairo.
Sheikh Yahya Hussein baadae alirejea nchini Tanzania mwanzoni mwa miaka ya sitini na kuanza shughuli zake za utabiri wa elimu ya nyota akiwa mtabiri wa mwanzo kabisa kueneza shughuli za utabiri wa nyota katika magazeti mbalimbali ya ukanda wa Afrika Mashariki.
Mnajimu huyo, amewahi kuendesha shughuli zake katika nchi za Afrika Mashariki na maeneo mengine duniani.
Pamoja na elimu yake ya unajimu, vile vile Sheikh Yahya Hussein alikuwa kiongozi wa dini ambaye pia alijihusisha na uchambuzi wa masuala ya siasa kupitia utabiri hususan wakati wa uchaguzi, ingawa hakushiriki kikamilifu katika kuwania nyadhifa zozote za kisiasa.
Pia alivuma sana katika kutabiri matokeo ya mechi kubwa za soka katika michuano ya Gossage na hata timu za Simba na Yanga za Tanzania bila kusahau vifo vya watu mashuhuri kama wanasiasa na wasanii pamoja na matukio makubwa duniani.
Marehemu Yahya Hussein ameacha mjane na watoto wapatao ishirini.

0 comments:

WELCOME URARY95 SPORTS NEWS BLOG | ADVERTISE YOUR BUSINESS HERE AT A CHEAP PRICE MORE INFORMATION CONTACT US: 0654315901 | Email: urary95@yahoo.com | KARIBU URARY95 SPORTS NEWS BLOG | TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA GHARAMA NAFUU KWA MAELEZO ZAIDI WASILIANA NASI: 0654315901 | Barua Pepe: urary95@yahoo.com
 
Back to top!