Searching...
Thursday, April 14, 2011

Kufichuliwa nyaraka zinazoonyesha jinsi Waingereza walivyowatesa Wakenya

 Mahakama Kuu ya London imefichua nyaraka zinazothibitisha namna wanamapinduzi wa Mau Mau nchini Kenya walivyoteswa na wanajeshi katili wa Uingereza wakati wa kupigania uhuru wan chi yao katika muongo wa 50.
Nyaraka hizo zinaonyesha namna wanajeshi wa utawala wa kikoloni wa Uingereza walivyowachoma moto Wakenya wakiwa hai. Aidha nyaraka hizo zinafichua namna Kamishna wa Polisi Kenya wakati huo Kanali Arthur Young anavyosimulia mauaji ya kikatili katika kambi za kuwashikilia wapigania uhuru. Moja ya nyaraka hizo zilizotayarishwa na Gavana wa Kenya mwaka 1955 Sir Evelyn Baring zinaonyesha namna wanajeshi wa Uingereza walivyompiga na kumchoma akiwa hai Mkenya mmoja mwanamapinduzi. Nyaraka hizo zimefichuliwa kufuatia kesi iliyofunguliwa London na Wakenya wanne walioteswa na utawala wa kikoloni wa Uingereza katika jitihada zake za kukandamiza harakati za kundi la kupigania uhuru wa Kenya la Mau Mau. Wakenya hao walio na umri wa zaidi ya miaka 80 wanataka serikali ya Uingereza iombe radhi na iwalipe fidia wanaharakati wote wa Mau Mau waliouawa katika muongo wa 50. Kamisheni ya Haki za Binadamu nchini Kenya imesema kuwa zaidi ya Wakenya 90,000 waliteswa au kuuawa na watu 160,000 waliwekwa kizuizini katika mazingira ya kuogofya. Kesi hiyo ya kihistoria inatazamiwa kufichua faili za jinai za kinyama za wakoloni Waingereza nchini Kenya.

0 comments:

WELCOME URARY95 SPORTS NEWS BLOG | ADVERTISE YOUR BUSINESS HERE AT A CHEAP PRICE MORE INFORMATION CONTACT US: 0654315901 | Email: urary95@yahoo.com | KARIBU URARY95 SPORTS NEWS BLOG | TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA GHARAMA NAFUU KWA MAELEZO ZAIDI WASILIANA NASI: 0654315901 | Barua Pepe: urary95@yahoo.com
 
Back to top!