Searching...
Wednesday, February 2, 2011

Maandamano yazidi nchini Misri

Maelfu ya watu wameendelea na maandamano katika mji mkuu wa Misri, Cairo, huku maandamano hayo yakiingia siku ya saba.
Waandamanaji Misri
Waandamanaji wamepuuza amri ya serikali
Waandamanaji hao wanatoa wito wa kufanyika mgomo wa kitaifa kuanzia hapo kesho Jumanne.
Polisi wameagizwa kurejea kwenye barabara za mji wa Cairo walizoziacha siku ya Ijumaa, wakati yalipofanyika mandamanao makubwa ya kuipinga serikali.
Serikali ya Misri inasema Polisi wameagizwa kushirikiana na Jeshi.
Waandamanaji wanataka Rais Hosni Mubarak aondoke madarakani baada ya kutawala kwa muda wa miaka 30.
Amejaribu kutuliza ghasia kwa kuahidi mabadiliko ya kisiasa, na akamwagiza waziri mkuu mpya Ahmed Shafiq kuharakisha mabadiliko ya kidemokrasia ili kubuni nafasi mpya za kazi.
Lakini waandishi wanasema ishara zote zinaonyesha mabadiliko pekee yatakayokubalika na waandamanaji ni Rais Mubarak kuondoka madarakani.
Mwandishi wa BBC anasema waandamanaji wengi bado wanaghadhabishwa na jaribio la Polisi kutumia nguvu kuzima maandamano.
Waandamanaji hao wameripotiwa kuzidisha harakati zao huku wakitoa wito wa kufanyika mgomo wa kitaifa na maandamanao makubwa mjini Cairo siku ya Jumanne.
Mjini Cairo kwenyewe helikopta za kijeshi zimeendelea kuzunguka angani karibu na bustani ambapo maelfu ya watu walikusanyika licha ya amri ya kutotoka nje usiku iliyotangazwa na serikali.
Jeshi limeripotiwa kuimarisha vituo vya ukaguzi kote mjini Cairo.
Wakati huo huo, Rais wa Misri Hosni Mubarak amefanya mabadiliko zaidi katika serikali yake huku wasi wasi ukiongezeka kuhusu athari za maandamano hayo juu ya uchumi wa nchi.
Taarifa zinasema Rais Mubarak amembadilisha waziri wa fedha Youssef Boutros-Ghali.
Hatua hiyo inakuja baada ya shirika moja la kimataifa la kukadiria uchumi kushusha viwango vya uthabiti wa uchumi wa Misri hadi chini ya sufuri.
Pia kuna taarifa kwamba waziri wa mambo ya ndani Habib al Adly ameondolewa na nafasi hiyo kuwekwa mtu mwingine.
Maelfu ya raia wa kigeni walioko mjini Cairo wanaendelea kusafirishwa kurudishwa makwao.
Raia wa kigeni waondoka Misri
Raia wa kigeni waliokwama katika uwanja wa ndege Cairo
Kundi la kwanza la raia wa Marekani wanasafirishwa leo kutoka Cairo kupelekwa nchini Cyprus, katika mwanzo wa mpango ulioanzishwa na Marekani.
Uchina, Japan na Australia pia zimetuma ndege kuwachukua raia wao huku kukiwa na taarifa kwamba mamia ya raia wa kigeni wamekwama kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa mjini Cairo.
New Zealand imesema huenda ikatumia usafiri wa kijeshi kuwahamisha raia wake kutoka Misri.
Nchi nyingi duniani zimewatahadharisha raia wao dhidi ya kusafiri kwenda Misri.

0 comments:

WELCOME URARY95 SPORTS NEWS BLOG | ADVERTISE YOUR BUSINESS HERE AT A CHEAP PRICE MORE INFORMATION CONTACT US: 0654315901 | Email: urary95@yahoo.com | KARIBU URARY95 SPORTS NEWS BLOG | TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA GHARAMA NAFUU KWA MAELEZO ZAIDI WASILIANA NASI: 0654315901 | Barua Pepe: urary95@yahoo.com
 
Back to top!