Searching...
Friday, June 11, 2010

HATIMAYE YAMETIMIA...

JO’BURG, Afrika Kusini
ILIKUWA miaka, miezi, siku, saa, sekunde hatimaye yametimia, fainali za Kombe la Dunia 2010 zinaanza leo nchini hapa.
Wakati sherehe za ufunguzi wa Kombe la Dunia 2010 zikiwa zimeanza tangu jana, leo hii michuano hiyo ndiyo inaanza rasmi kwa kushirikisha nchi 32.
Hii ni historia ya aina yake katika soka kwa Afrika kwa kubeba jukumu la uenyeji wa michuano hii mikubwa kuliko yote kwa soka ulimwenguni.

Ukitoa wenyeji Afrika Kusini, mataifa mengine yanayochuana katika michuano hii ni Mexico, Ufaransa, Uruguay (kundi A), kundi B kuna timu za Argentina, Ugiriki, Nigeria na Korea Kusini. Kundi C zipo Algeria, England, Slovenia na Marekani. Australia, Ujerumani, Ghana na Serbia zipo kundi D huku Cameroon, Denmark, Uholanzi na Japan zikiwa kundi E.
Mabingwa watetezi Italia, New Zealand, Paraguay na Slovakia zipo kundi F, kundi G lina timu za Brazil, Ivory Coast, Korea Kaskazini na Ureno huku kundi H kuna Chile, Honduras, Hispania na Uswisi.

BURUDANI NA UFUNGUZI:
Wengi wanafahamu kwamba leo ndiyo siku ya ufunguzi wa fainali za Kombe la Dunia, lakini jana Alhamisi kulifanyika tamasha la aina yake la uzinduzi wa michuano hii.
Nyota mbalimbali wa muziki akiwemo Shakira walitarajiwa kutumbuiza jana Alhamisi katika tamasha hilo maalum lililofanyika katika Uwanja wa Orlando unaoweza kuchukua watazamaji 40,000. Uwanja huu upo katika kitongoji maarufu cha Soweto jijini Johannesburg.
Shakira wa Colombia ambaye wimbo wake wa ‘Waka Waka’ (This Time for Africa-Ni wakati wa Afrika) ulio katika mahadhi ya samba ndiyo maalum kwa michunao hiyo uliopitishwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), alipangwa kutumbuiza mara mbili, yaani jana Alhamisi na leo Ijumaa katika ufunguzi rasmi wa michuano hii.

Mwanamuziki huyo alisema, “Nina furaha kwamba wimbo wa Waka Waka umechaguliwa kuwa sehemu ya Kombe la Dunia 2010.”
“Kombe hili la Dunia la Fifa ni moja kati ya vitu vya muhimu duniani, linaunganisha kila nchi, itikadi, dini na hali yoyote ya kila mtu. Ni tukio linaloweza kuunganisha watu, hiki ndicho kinachoelezwa ndani ya wimbo wangu,” alisema.
Mwanamuziki huyo anaimba wimbo huo kwa kushirikiana na kundi la pop la Afrika Kusini la Freshlyground, lakini pia wanamuziki kama John Legend, Alicia Keys, kundi la Black Eyed Peas, na muimbaji wa rock kutoka Colombia, Juanes. Wengine ni wa kutoka Afrika ambao ni Amadou na Mariam, Angelique Kidjo na kundi la Parlotones.

Kama ilivyo kwa sherehe za leo ambazo zitaambatana na mechi ya ufunguzi kati ya wenyeji na Mexico, Fifa awali haikufafanua zaidi namna utaratibu ulivyopangwa katika tamasha la jana. Tiketi za tamasha hilo zilikuwa zikiuzwa kwa rand 1,400 (ambazo ni sawa na dola 200 za Marekani- pia sawa na Sh. 250,000).
Lakini wakati hayo yakitokea, Lebo M, ambaye ni mzaliwa wa Soweto anatarajiwa pia kutumbuiza leo hii ndani ya muda wa dakika 25 uliotengwa kwa burudani kwenye Uwanja wa Soccer City. Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela ameuchagua wimbo wa “Hope” wa mtindo rock uliopigwa na Russ Ballard na Chris Winter uimbwe leo.

DAKIKA 15 ZA MANDELA SOCCER CITY:
Mzee Mandela ameripotiwa kuhudhuria sherehe hizo za ufunguzi katika Uwanja wa Soccer City lakini kwa muda mfupi.


Mmoja wa wajukuu wa Rais huyo wa zamani wa Afrika Kusini aliyekaa jela kwa muda wa miaka 28 kudai uhuru wa nchi hiyo, alisema Mandela amekubali kuhudhuria sherehe hizo lakini akatoa agizo la kukaa kwa muda mfupi na si vinginevyo, japokuwa wapo katika hatua za kumshawishi kuwapo uwanjani zaidi ya muda huo.

SHULE ZAFUNGWA:
Nchini Swaziland hasa katika jiji la Mbabane, Chama cha Wakuu wa Shule wa Swaziland (Swapa), kimesema kwamba kina matumiani kwamba, wanafunzi watakosa masomo kwa ajili ya kupata muda wa kutazama mechi za Kombe la Dunia linaloanza leo.
Katibu Mkuu wa Swapa, Charles Bennett alisema wakuu wa shule wameamua kutenga baadhi ya siku ambazo wanafunzi hawatokwenda shule kuhudhuria masomo yao, ili kupata muda wa kubaki nyumbani au kwingineko kutazama mechi za Kombe la Dunia kupitia runinga.
Kwa mfano, leo hii wanafunzi wengi wataruhusiwa mapema ili waweze kufuatilia kwa makini sherehe za ufunguzi na mechi ya Afrika Kusini na Mexico.

Bennett alisema michuano ya Kombe la Dunia ni kitu kinachofanyika kihistoria, hivyo wanafunzi wanatakiwa kupewa muda wa kutazama michuano hiyo. Shule nyingi za sekondari za Swaziland huwa zinamaliza masomo saa 11:00 jioni huku shule za msingi zikifanya hivyo saa 9:00 alasiri. Mechi za Kombe la Dunia zinachezwa katika muda uliogawanyika katika sehemu tatu ambazo ni saa 8:30 mchana, saa 11:00 jioni na saa 3:30 usiku.
Leo hii mara baada ya ufunguzi, Afrika Kusini itacheza na Mexico saa 11:00 jioni katika Uwanja wa Soccer City ikiwa ni mechi ya kwanza ya michuano hii. Baadaye saa 3:30 usiku Ufaransa itacheza na Uruguay.
“Shule zitakuwa na runinga. Lazima wajipange vizuri ili waweze kutazama. Lakini hatutarajii kupata usumbufu mkubwa,” alisema Mkuu wa shule ya Manzini Central.

MSHTUKO WA WAALIKWA:
Wakati Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma amemwalika Rais wa Chama cha Congress cha India, Sonia Gandhi, ili kutazama Kombe la Dunia 2010, awali zilikuwapo habari za ujio wa Rais wa Marekani, Barack Obama na Mfalme Mswati III wa Swaziland.
Pia kuna habari za kualikwa kwa mastaa mbalimbali wa Bollywood akiwamo Bipasha Basu, ambaye anaelezwa kuwa ni shabiki mkubwa wa soka na ameshaonesha nia yake ya kutazama baadhi ya mechi za Kombe la Dunia hasa fainali au nusu fainali.
Lakini pamoja na matarajio haya ya kuwapo kwa viongozi hawa, ni Mswati peke yake aliye na asilimia nyingi za kuhudhuria ufunguzi wa michuano hiyo na hata baadhi ya mechi. Gandhi na Obama hawajathibitisha na kuna wakati maofisa wa usalama wa Afrika Kusini walitamania kiongozi huyo wa Marekani asihudhurie fainali hizo kwa kuhofia bugudha ya ulinzi ambayo wangeipata.

MECHI YA UFUNGUZI:
Leo kutakuwa na mechi mbili za ufunguzi, lakini mchezo kati ya Afrika Kusini na Mexico ndiyo unaopewa uzito mkubwa japokuwa Ufaransa itacheza na Ufaransa baadaye.
Kama mchezo wa Afrika Kusini na Mexico ungechezwa katika ‘uwanja huru’, Mexico ingeweza kupewa nafasi ya kushinda mechi hii. Tangu ilipotangazwa kucheza mechi ya kwanza ya michuano hii na kucheza katika Uwanja wa Soccer City jijini Johannesburg, dhidi ya wenyeji, Mexico walijawa na presha ya hali ya juu. Kwao ni hatari kucheza mchezo wa kwanza dhidi ya wenyeji.

Mexico chini ya Kocha Javier Aguirre, imecheza mechi 12 za kirafiki ili kujianda na Kombe la Dunia huku nusu ya mechi hizo zikihusisha timu zinazoshiriki michuano hii. Ana imani kubwa na kikosi chake katika michuano hii.
Kwa upande wake Afrika Kusini, kocha Carlos Parreira atakuwa na presha ya kutotaka kuwa wa kwanza kutoka katika hatua ya makundi huku akiwa mwenyeji.
Afrika Kusini bado ina jinamizi la kutolewa katika hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika iliyofanyika Angola mapema mwaka huu

WACHEZAJI WA KUTAZAMWA ZAIDI:
Giovani Dos Santos anatarajiwa kuwa tegemeo la Mexico; huyu anatarajiwa kuisaidia timu yake kuvuka hatua ya makundi pia kuingia katika timu nane zitakazocheza robo fainali.
Steven Pienaar, ndiye anayetarajiwa kuwa nyota wa Afrika Kusini badala ya Benn McCarthy ambaye ametemwa. Huyu atakuwa na wajibu wa kuunganisha mipira kutoka nafasi ya kiungo hadi kwa washambuliaji.

ITAKAVYOKUWA:
Mexico inaweza kufanya vizuri endapo itawatoa akilini mashabiki wengi watakaowapigia kelele za vuvuzela. Soccer City unaweza kuwa mwanzo mzuri wa Afrika Kusini katika harakati zake za kutwaa Kombe la Dunia. Mbali ya kuwa chini ya Parreira . Kama Mexico ikiwa mbele kwa mabao mawili hadi mapumziko, inaweza kushinda mabao 3-1 mwishoni, lakini wakiiacha Afrika Kusini kuongoza hadi mapumziko, wanaweza kuingia katika matatizo
Habari na Globalpublisher

0 comments:

WELCOME URARY95 SPORTS NEWS BLOG | ADVERTISE YOUR BUSINESS HERE AT A CHEAP PRICE MORE INFORMATION CONTACT US: 0654315901 | Email: urary95@yahoo.com | KARIBU URARY95 SPORTS NEWS BLOG | TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA GHARAMA NAFUU KWA MAELEZO ZAIDI WASILIANA NASI: 0654315901 | Barua Pepe: urary95@yahoo.com
 
Back to top!