Umoja na Mshikamano wasisitizwa kwenye kongamano la Hija nchini Tanzania
Kongamano la siku mbili la Hija limeanza mjini Dar es Salaam Tanzania kwa kuwataka Waislamu wahifadhi na walinde umoja na mshikamano wao. Kongamano hilo ambalo linahudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi 14 za eneo la mashariki, kusini na katikati mwa bara la Afrika, limeandaliwa na Be'etha ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, kwa kushirikiana na Ubalozi wa Iran mjini Dar es Salaam, Baraza Kuu la Waislamu nchini Tanzania BAKWATA na Be'etha ya Mahujaji nchini Tanzania. Kwenye hotuba ya ufunguzi, Sayyid Ali Qadhi Askari Mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu katika masuala ya Hija amesema kuwa, Iran ikiwa na uzoefu mkubwa wa masuala ya hija, iko tayari kutoa ushirikiano na uzoefu wake kwa nchi nyingine za Kiislamu katika uwanja huo. Amesema kuwa, lengo la kuitishwa kongamano hilo ni kuimarisha mshikamano wa Kiislamu, kwa kuzingatia kuwa hija ni nembo ya umoja wa Kiislamu. Kongamano hilo la siku mbili ambalo linafikia kilele chake leo Jumatatu, linahudhuriwa na shakhsia mbalimbali wakiwemo Mehdi Mustafawi Mkuu wa Taasisi ya Utamaduni na Mawasiliano ya Kiislamu ya Iran, Sheikh Muhammad Akhtari Mkuu wa Taasisi ya Kimataifa ya Ahlul Bayt AS, Alhaj Ali Hassan Mwinyi Rais mstaafu wa Tanzania, mawaziri na viongozi mbalimbali wa dini ya Kiislamu.
0 comments:
Post a Comment