Baraza Kuu la Maaskofu la Vatican linaloshughulikia masuala ya mazungumzo kati ya dini mbalimbali limetoa ujumbe wa kulaani vikali mikakati ya Askofu Terry Jones ya kutaka kuteketeza Qurani Tukufu wakati wa kuwadia tarehe Septemba 11. Baraza la Vatican limeeleza kuwa, kitendo hicho ni cha hatari kwani Qurani Tukufu ni kitabu kitakatifu kwa jamii ya Waislamu. Baraza Kuu la Maaskofu la Vatican limeeleza kitendo cha Askofu Jones ni cha kipumbavu na wala hakipaswi kupuuzwa na kufumbiwa macho.
Wakati huohuo, Sheikh Abdul Muatwi al Buyumi mjumbe wa jopo la wasomi katika Chuo Kikuu cha al Azhar nchini Misri amesema kuwa, kuna uwezekano mkubwa wa kuingia dosari uhusiano wa Marekani na ulimwengu wa Kiislamu iwapo Askofu Jones atatekeleza uamuzi wake wa kuteketeza Qurani. Amesema kuwa, kama Marekani itashindwa kuzuia uteketezwaji huo wa Qurani, kitendo hicho kitahesabiwa kuwa ni ugaidi mkubwa wa kidini. Kwa upande mwingine, Amr Mussa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kiarabu amelaani vikali mpango wa Askofu Terry Jones mwenye misimamo ya kufurutu ada wa nchini Marekani wa kutaka kuchoma moto nakala kadhaa za Qurani Tukufu katika siku ya tarehe 11 Septemba. Amru Mussa ameongeza kuwa, wananchi walio wengi wa Marekani wanapinga kitendo hicho kisicho cha kibinadamu ambacho bila shaka kitakuwa na matokeo mabaya katika siku zijazo nchini humo. Mpango wa kundi la Kikristo linaloitwa Dove World Outreach Center lenye makao yake katika jimbo la Florida, umezusha mtafaruku mkubwa ulimwenguni na hasa katika ulimwengu wa Kiislamu. Serikali ya Marekani imeueleza mpango huo kuwa hatari kwa wanajeshi wao walioko nchini Afghanistan na kusisitiza kuwa, mpango huo unahuisha uadui wa Marekani katika nchi za Kiislamu. Kwa upande wake, Catheline Ashton Mkuu wa Siasa za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amelaani vikali mpango huo wa Askofu Terry Jones wa kutaka kuziteketeza nakala kadhaa za Qurani Tukufu, na kusisitiza juu ya ulazima wa kuheshimiwa itikadi zote za kidini.
0 comments:
Post a Comment