Katika kizazi kimoja, tumeshuka kutoka nafasi ya kwanza hadi nafasi ya 12 kwenye viwango vya kuhitimu kwa vijana katika vyuo vikuu.
Akihutubia umati wa watu walokuwa na furaha kwenye chuo kikuu cha Texas, Jumatatu, rais Obama alisema Marekani haiwezi kamwe kupuuzi mwenendo unaokera katika elimu ya juu.
“Tumekuwa tukirudi nyuma. Katika kizazi kimoja, tumeshuka kutoka nafasi ya kwanza hadi nafasi ya 12 kwenye viwango vya kuhitimu kwa vijana katika vyuo vikuu. Hilo halikubaliki, lakini linaweza kubadilishwa. Tunaweza kuchukuwa tena uwongozi.” alisema rais Obama.
Rais alisema mafanikio katika elimu na ukuwaji wa kiuchumi ni mambo yanayoingiliana, hasa katika uchumi wa dunia unoendeshwa na teknolojia na habari yani teknohama. Lengo lake ni kuona wanafunzi milioni 8 zaidi wanahitimu kutoka vyuo vya Marekani ifikapo mwaka 2020.
“Elimu ni suala la kiuchumi. Elimu ni suala la kiuchumi la wakati wetu. Ni suala la kiuchumi pale kiwango cha ukosefu wa ajira kwa watu ambao hawajawahi kuhudhuria vyuo vikuu imeongezeka maradufu, ya idadi ya wale walohudhuria vyuo vikuu. Elimu ni suala la kiuchumi wakati kila ajira nane kati ya kumi itahitaji aidha uwe na ujuzi fulani au, uwe umetimiza elimu ya juu ifikapo mwisho wa muongo huu. Elimu ni suala la kiuchumi pale tunapofahamu bila ya shaka, kuwa nchi ambazo zilizotupita kielimu hii leo, zitatushinda hapo kesho." alisema rais Obama.
Bw. Obama alisema walipokuwa vijana, wote yeye na mkewe Michele Obama, walipambana na hali ya kulipa mikopo yao ya shule. Alisema nafasi za elimu hazifai kuwekewa vikwazo kutokana na uwezo wa kifedha wa familia. Rais alisema kuwa serikali kuu imebadilisha mfumo wa kutoa mikopo kwa wanafunzi, huku ikipunguza kodi kwa familia zinoshindwa kulipa gharama za shule. Wakati huo huo, rais alisema juhudi lazima ziendelee kuzidisha idadi za wanafunzi wanohitimu vyuo vikuu.
Rais Obama alikiri kuwa Marekani inkabiliwa na wakati mgumu kiuchumi, na kwamba baadhi ya wanafunzi huwenda wakahoji ikiwa ni jambo la busara kuendelea na elimu ya juu wakati ambapo soko la ajira liko dhaifu. Lakini rais alisema uwezekano wa hali ya uchumi kunawiri, itawezekana tu, kukiwepo wafanyakazi waloelimika, na kwamba wanafunzi wa leo wanabeba matumaini kwa hali bora ya kesho.
Kwa miongo kadhaa mfumo wa elimu ya juu marekani, umekuwa mojawapo ya mifumo ilo bora zaidi duniani. Lakini katika miaka ya karibuni, kiwango cha wamarekani wenye vyeti vya vyuo vikuu kimepunguka, wakati ambapo gharama za shule za kitaifa na za kibinafsi zimeongezeka.
Habari na Sauti ya Amerika
0 comments:
Post a Comment