China sasa ni nchi ya pili yenye nguvu kubwa zaidi za kiuchumi duniani
Baada ya miongo mitatu ya ukuaji mkubwa wa kiuchumi, China imeipita Japan na kuwa nchi ya pili baada ya Marekani yenye uwezo mkubwa zaidi wa kiuchumi duniani. Takwimu zilizotolewa na serikali ya Japan zimeeleza kuwa ulimwengu utashuhudia dola jipya lenye nguvu kubwa za kiuchumi baada ya utafiti kuonyesha kuwa katika kipindi cha miezi mitatu ya pili ya mwaka huu wa 2010, pato la kiuchumi la China lilikuwa ni dola trilioni 1.33 kulinganisha na Japan ambayo pato lake lilikuwa ni dola trilioni 1.28. Kwa muda wa zaidi ya miaka 40 Japan ilikuwa ndio dola la pili lenye nguvu kubwa zaidi za kiuchumi duniani baada ya Marekani, lakini uchumi wa nchi hiyo ulidorora katika muongo wa 1990. Licha ya uchumi wa dunia kudorora kutokana na mtikisiko wa kiuchumi, uchumi wa China umekuwa ukikuwa kwa asilimia 10 kwa mwaka. Wataalamu wa uchumi wanatabiri kuwa mnamo mwaka 2030 China itaipita hata Marekani na kuwa dola lenye nguvu kubwa zaidi za kiuchumi duniani.
0 comments:
Post a Comment