Ban Ki Moon amteua Mkenya kusimamia ofisi mpya ya UN nchini Ethiopia
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amemteua mwanadiplomasia wa Kenya kusimamia ofisi mpya ya umoja huo iliyoko mjini Addis Ababa nchini Ethiopia. Zachary Muburi Muita ambaye tangu mwaka 2006 amekuwa balozi wa kudumu wa Kenya kwenye Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani sasa atakuwa na jukumu la kuimarisha uhusiano kati ya umoja huo na Umoja wa Afrika. Ofisi hiyo mpya ya UN mjini Ethiopia ilianzishwa mapema mwaka huu ili kutoa nafasi kwa AU na UN kuchanga bia katika kutatua matatizo yanayolikabili bara la Afrika. Addis Ababa pia ndiyo makao makuu ya Umoja wa Afrika AU. Taarifa kutoka ofisi ya Ban Ki Moon imesema kuwa pana haja ya kuwepo ushirikiano wa karibu kati ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika ili bara la Afrika liweze kufikia kilele cha msaada na ufanisi.
0 comments:
Post a Comment