Viongozi wa mataifa ya Afrika wamewasili Kampala katika nyakati mbali mbali tayari kwa mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika, AU, unaotazamiwa kuanza Jumapili.
Ujumbe mkuu wa mkutano huo ni Afya ya Wazazi, Watoto na Maendeleo Afrika ikiwa ni sehemu ya malengo la milenia ya Umoja wa Mataifa ambayo wanachama wote 53 wa Umoja Afrika wanatazamia kuyatekeleza.
Serikali ya Uganda imeeneza ulinzi mkali mjini Kampala katika kipindi hiki cha kuhudhuria kwa viongozi hao. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda Okello Oryem alisema Jumamosi ulinzi uko katika hali ya juu kuliko wakati wa ziara nyingine za viongozi kutoka nje ya nchi.
Mkutano huo unaanza Jumapili, wiki mbili tangu watu 76 wafariki kufuatia milipuko ya mabomu mawili wakati watu wanaangalia fainali ya kombe la dunia katika televisheni Julai 11.
Kundi la Somalia la al-shabab lilidai kuhusika katika shambulizi hilo likisema ilikuwa kisasi kwa Uganda kupeleka wanajeshi katika jeshi la ulinzi wa amani ya Umoja wa Afrika huko Somalia.
Habari na Sauti ya Amerika
0 comments:
Post a Comment