Rais Hosni Mubarak wa Misri jumanne usiku alitangaza kwa njia ya televisheni kuwa hatagombea urais katika uchaguzi utakaofanyika mwezi Septemba mwaka huu. Pia amelitaka bunge lifanye marekebisho ya vifungu husika vya katiba vinavyoweka masharti kwa mgombea rais na vile vinavyobainisha kipindi cha urais. Rais Mubarak amesema katika miezi iliyobaki ya kipindi chake, atachukua hatua zinazohitajika kuhakikisha kupokezana madaraka katika hali ya utulivu, serikali inaendelea kufanya kazi na madai halali ya wananchi yanatimizwa. Pia amezitaka idara za usimamizi na uendeshaji wa mashitaka ziwachukulie hatua wahusika wa ufisadi, na wale wanaofanya vurugu hivi sasa.
Katiba ya sasa ya Misri inamruhusu rais kugombea urais bila ukomo, na kipindi cha urais kwa awamu moja ni miaka 6.
Rais Barack Obama wa Marekani siku hiyo baada ya kuongea na rais Mubarak kwa njia ya simu alisema, mchakato wa kupokezana madaraka nchini Misri ni lazima uanze sasa, na ni lazima uwe wa amani na wenye maana.
Habari nyingine zinasema huduma za Internet nchini Misri ambazo zilisimamishwa na serikali siku 8 zilizopita zimepatikana tena jumatano mchana.


0 comments:
Post a Comment