Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika limetayarisha rasimu ya azimio la kupiga vita ugaidi kwa ajili ya nchi 53 wanachama wa umoja huo. Azimio hilo linapiga marufuku harakati zote za kigaidi na uharamia unaofanyika kwa ajili ya kuchukua vikomboleo barani humo. Rasimu ya azimio la kupambana na ugaidi barani Afrika inachunguzwa katika kikao cha wataalamu wa Umoja wa Afrika ambacho kinafanyika leo na kesho Jumatano tarehe 15 Disemba katika mji mkuu wa Algeria, Algiers.
Karibu wageni 200 wanashiriki katika kikao hicho ambacho pia kinahudhuriwa na marais wa zamani wa Afrika Kusini na Nigeria Thabo Mbeki na Olusegun Obasanjo, Kamishna wa Usalama na Amani wa Umoja wa Afrika Ramtane Lamamra, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Jean Ping, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Amru Mussa na mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon. Wataalamu wa Umoja wa Afrika wako chini ya Kituo cha Utafiti na Uhakiki kinachochunguza masuala ya ugaidi cha umoja huo ambacho kilianzishwa mwaka 2004 mjini Algiers.
Kazi kuu ya taasisi hiyo ni kuimarisha uwezo wa nchi za Afrika kwa ajili ya kuzuia harakati za kigaidi barani humo.
Baada ya kupasishwa rasimu hiyo nchi za Kiafrika zitakuwa na uwezo wa kisheria wa kuwafuatilia na kuwatia nguvuni washukiwa wa operesheni za kigaidi katika nchi zao.
Kamishna wa Usalama na Amani wa Umoja wa Afrika Ramtane Lamamra amesema kuwa kumefanyika juhudi za kuoanisha kati ya mada za rasimu hiyo na sheria za nchi za Kiafrika. Baada ya uchunguzi wa mada zake, rasimu hiyo itawasilishwa kwa viongozi wa nchi wanachama kwa ajili ya kupasishwa. Viongozi hao pia watatakiwa kuwasilisha faharasa ya majina ya washukiwa maarufu wa operesheni na vitendo vya kigaidi na vilevile taasisi na makundi ya kigaidi.
Katika miaka ya hivi karibuni eneo la pwani mwa kaskazini magharibi mwa Afrika linalojumuisha nchi za Algeria, Mali, Niger na Mauritania limeshuhudia ongezeko la harakati kubwa za magendo na utoroshaji wa dawa za kulevya. Vilevile kundi la al Qaida magharibi mwa Afrika limekuwa likiteka nyara raia wa kigeni katika eneo hilo. Tarehe 17 Disemba mwaka uliopita Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio lililopiga marufuku fidia na vikomboleo vinavyotolewa kwa makundi ya kigaidi yanaoteka nyara raia wa kigeni. Umoja wa Afrika pia tarehe 3 Julai mwa jana ulipasisha azimio linaloshabihiana na hilo.
Vitendo vya kuteka nyara meli za kibiashara na za starehe vimekithiri mno katika eneo la Pembe ya Afrika na Ghuba ya Aden. Harakati hizo zinaendeswa na maharamia wa pwani mwa Somalia. Huko Magharibi mwa Afrika makundi ya waasi yamekuwa yakiteka nyara watu hususan wafanyakazi wa makampuni makubwa ya mafuta ya nchi za kigeni.
Inatarajiwa kuwa rasimu ya sasa ya Umoja wa Afrika itasaidia kupunguza vitendo kama hivyo vya uhalifu na kuzipa nchi za Kiafrika uwezo mkubwa zaidi wa kukabiliana na makundi hayo.


0 comments:
Post a Comment