Searching...
Thursday, December 30, 2010

Jela kwa kushambulia wachezaji wa Togo

Mahakama moja nchini Angola imemhukumu kwenda jela miaka 24 mtuhumiwa wa shambulio la timu ya taifa ya soka ta Togo, mwezi Januari.
Cabinda
Cabinda
Mtuhumiwa huyo ni Joao Antonio Puati. Wakili wa mtuhumiwa huyo ameliambia shirika la habari la AFP kuwa alikutwa na hatia ya kufanya "uasi kwa kutumia silaha".
Basi lililokuwa limebeba timu hiyo, lilishambuliwa katika jimbo la Cabinda, wakati wachezaji hao wakielekea katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika.
Jeneza
Jeneza la mmoja wa maafisa waliouawa wa Togo
Bw Puati alikana mashitaka hayo, na amekanusha kuhusiana na kundi la waasi ambalo lilidai kuhusika na shambulio hilo.
Mtu mwingine, Daniel Simbai, alifutiwa mashitaka kama hayo, yaliyokuwa yakimkabili.

Alikuwepo

Maafisa wawili wa Togo waliuawa, katika shambulio hilo lililodumu kwa nusu saa, ambalo kundi la waasi la Flec linadai kuhusika nalo.
"Joao Antonio Puati alikuwepo katika eneo la tukio, na uhusiano wake na Flec umeonekana wakati wa kesi," amesema mwendesha mashitaka mkuu wa Cabinda, Antonio Nito, wakati akizungumza na AFP.
Mwandishi wa zamani wa BBC nchini Angola Louise Redvers amesema mawakili wa upande wa utetezi wamekata rufaa katika mahakama kuu.
Cabinda
Emmanuel Adebayor akipozwa na mchezaji mwenzake
Wamesema ushahidi wa uhusiano na kundi la Flec haukuoneshwa wakati kesi ikiendeshwa, bali ulitokana na taarifa za polisi zilizochukuliwa kutoka kwa Puati wakati akiwa kizuizini.
Wakili wa utetezi Arao Tempo ameiambia BBC kuwa mteja wake aliteswa wakati akiwa jela la kulazimishwa kukiri kuwa anahusiana na Flec.

Kisiasa

Amesema uamuzi wa kumhukumu Bw Puati ambaye ni raia wa Kongo-Brazzaville, na kumuachilia huru mtuhumiwa mwenzake ambaye ni raia wa Angola, ni wa kisiasa.
Amesema hukumu hiyo ni kupeleka ujumbe Kongo-Brazzaville, ambako waasi wengi na wafuasi wa Flec wanaishi na kufanya shughuli zao.

Gerezani

Wiki iliyopita, wanaharakati wanne wa haki za binaadam waliokamatwa kuhusiana na shambulio hilo la mwezi Januari, waliachiliwa huru kutoka gerezani.
Makundi ya haki za binnadam yameituhumu Angola kwa kutumia shambulio dhidi ya timu ya Togo, ili kuhalalisha msako dhidi ya wakosoaji wa serikali katika jimbo la Cabinda.
Flec imekuwa ikipigana kwa miongo mitatu kudai uhuru wa Cabinda, eneo ambalo linatenganishwa na Angola kwa kipande kidogo cha ardhi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Licha ya eneo hilo kuwa na utajiri wa mafuta, ni moja ya maeneo masikini zaidi nchini Angola.

0 comments:

WELCOME URARY95 SPORTS NEWS BLOG | ADVERTISE YOUR BUSINESS HERE AT A CHEAP PRICE MORE INFORMATION CONTACT US: 0654315901 | Email: urary95@yahoo.com | KARIBU URARY95 SPORTS NEWS BLOG | TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA GHARAMA NAFUU KWA MAELEZO ZAIDI WASILIANA NASI: 0654315901 | Barua Pepe: urary95@yahoo.com
 
Back to top!