Searching...
Friday, December 17, 2010

Baraza la Usalama lawaonya wanaokandamiza watu nchini Ivory Coast.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa onyo kali kwa makundi yanayokandamiza watu nchini Ivory Coast likisema kuwa sheria za kimataifa zitayaandama makundi hayo. Onyo hilo limetolewa na wanachama wa Baraza la Usalama baada ya kusikiliza ripoti ya Allen Ray msimamiaji wa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa huko Kodivaa ambaye amesema makumi ya watu wameuawa katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa inamtambua Allassane Ouattara kuwa mshindi wa uchaguzi wa kihistoria wa Rais wa Ivory Coast kama alivyotangazwa na tume ya uchaguzi ya nchi hiyo na imemtaka Laurent Gbagbo ambaye inaamini amepora ushindi huo, kukabidhi madaraka kwa Rais aliyechaguliwa na wananchi. Kwa mujibu wa taarifa za vyombo mbalimbali vya habari, watu wasiopungua 30 waliuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa katika machafuko yaliyotokea usiku wa kuamkia leo kwenye miji ya Abidjan na Yamoussoukro. Habari hizo zimeongeza kuwa kuwa vituo vya kibiashara na kiuchumi katika miji hiyo vimefungwa. Yamoussoukro ni mji mkuu wa kisiasa wa Kodivaa na ni eneo ambalo linatenganisha maeneo ya kaskazini na kusini mwa nchi hiyo. Katika mapigano ya ndani ya mwaka 2003, Ivory Coast iligawanyika sehemu mbili, sehemu ya kaskazini yenye wafuasi wa Ouattara na sehemu ya kusini inayodhibitiwa na wanamgambo wanaomuunga mkono Gbagbo. Hivi sasa kuna Marais na serikali mbili nchini humo. Alassane Ouattara anasema ni haki yake kuunda serikali kwani amechaguliwa na wananchi na kutangazwa mshindi na tume ya uchaguzi. Laurent Gbagbo naye amejitangazia ushindi baada ya Baraza la Katiba linalomuunga mkono kudai kuwa yeye ndiye aliyeshinda uchaguzi huo. Weledi wa mambo wanasema kuwa, hatua ya Gbagbo ya kutangazwa mshindi na kuapishwa haraka sana kuwa Rais wa Kodivaa inakumbushia hatua kama hiyo iliyowahi kuchukuliwa nchini Kenya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007. Weledi hao wanasema kuwa, hivi sasa kumezuka suna mbaya barani Afrika ya kuchukua madaraka kwa nguvu baada ya kushindwa katika uchaguzi na baadaye kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa kati ya pande hasimu baada ya kutokea machafuko na umwagaji wa damu. Yaliyotokea nchini Kenya na Zimbabwe ni mfano wa wazi wa suna hiyo na inaonekana jamii ya kimataifa haipendi kuona suna hiyo mbaya inaendelea. Kadiri muda unavyopita ndivyo mashinikizo dhidi ya Laurent Gbagbo yanavyozidi kuongezeka. Lililobaki ni kusubiri na kuona ni kiasi gani Gbagbo ataweza kustahamili mikiki ya mashinikizo ya ndani ya kimataifa na ni wapi utaelekea mustakbali tata wa Ivory Coast.

0 comments:

WELCOME URARY95 SPORTS NEWS BLOG | ADVERTISE YOUR BUSINESS HERE AT A CHEAP PRICE MORE INFORMATION CONTACT US: 0654315901 | Email: urary95@yahoo.com | KARIBU URARY95 SPORTS NEWS BLOG | TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA GHARAMA NAFUU KWA MAELEZO ZAIDI WASILIANA NASI: 0654315901 | Barua Pepe: urary95@yahoo.com
 
Back to top!