Searching...
Thursday, November 25, 2010

Hitilafu juu ya jinsi ya kugawana maji ya Mto Nile

 Viongozi wa Misri wamesisitiza juu ya udharura wa kutatuliwa hitilafu zilizopo kuhusu jinsi ya kugawana maji ya Mto Nile kwa njia ya mazungumzo. Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imetangaza kuwa nchi hiyo haina nia ya kuingia kwenye vita na nchi nyingine za kandokando ya Mto Nile. Hata hivyo Waziri Mkuu wa Ethiopia Meles Zenawi amesema kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kutokea vita juu ya maji ya Mto Nile.
Suala la kugawana maji ya Mto Nile kati ya nchi zenye vyanzo vya mto huo na za kandokndo yake lina historia ya muda mrefu. Burundi, Rwanda, Tanzania, Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Uganda na Ethiopia ni miongoni mwa nchi za kandokndo ya Mto Nile. Miezi kadhaa iliyopita nchi za Tanzania, Kenya, Ethiopita, Uganda na Rwanda zilitia saini makubaliano yanayosisitiza juu ya kugawana maji ya Mto Nile kwa uadilifu zaidi. Nchi hizo zinatarajia kuwa makubaliano hayo mapya yatachukua nafasi ya mkataba wa zamani uliotiwa saini katika kipindi cha ukoloni juu ya jinsi ya kugawana maji ya Mto Nile.
Makubaliano hayo ya zama za ukoloni yanazipa Misri na Sudan asilimia karibu 80 ya maji ya Mto Nile. Nchi hizo mbili pia zimepinga makubaliano mapya ya maji ya mto huo zikisema kuwa yanapingana na haki zao za kihistoria za kutumia maji ya Nile. Misri na Sudan zimetangaza kuwa zina uwezo wa kutosha wa kulinda haki zao.
Wataalamu wa mambo wanasema kuwa ongezeko la jamii katika nchi za kandokando ya Mto Nile ni miongoni mwa sababu kuu za mivutano na malalamiko yanayotolewa kuhusu ugawanaji wa maji ya mto huo. Kwa sasa hisa ya Misri peke yake ya maji ya Nile ni asimilia 55 na Sudan asilimia 18 huku nchi saba zilizosalia zikiambulia asilimia iliyobakia ambayo ni sawa na mita cubic milioni 680 za maji.
Baadhi ya wachambuzi wa mambo pia wanasema kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel umechangia katika kuchoche zaidi mivutano kati ya nchi za kandokando ya Mto Nile. Wataalamu hao wanasisitiza kuwa baada ya kutiwa saini mkataba wa Camp David kati ya Misri na Israel na kukataliwa ombi la Tel Aviv la kutumia sehemu ya maji ya Mto Nile, Wazayuni walianzisha mikakati ya kuimarisha zaidi uhusiano na nchi za kandokando ya mto huo. Wachambuzi hao wanasema tangu wakati huo Israel ilituma wataalamu wake katika nchi za Kenya, Tanzania, Rwanda, Burundi na Ethiopia na kuanza kutekeleza miradi ya aina mbalimbali inayohitajia maji mengi katika nchi hizo. Suala hilo kwa upande mwingine limezishawishi nchi husika kutaka mkataba wa kugawana maji ya Mto Nile uangaliwe upya.

0 comments:

WELCOME URARY95 SPORTS NEWS BLOG | ADVERTISE YOUR BUSINESS HERE AT A CHEAP PRICE MORE INFORMATION CONTACT US: 0654315901 | Email: urary95@yahoo.com | KARIBU URARY95 SPORTS NEWS BLOG | TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA GHARAMA NAFUU KWA MAELEZO ZAIDI WASILIANA NASI: 0654315901 | Barua Pepe: urary95@yahoo.com
 
Back to top!