“Ilikuwa kishindo kikubwa kuliko vyote nilivyopata kusikia katika maisha yangu, maumivu makali yalipita kifuani kwangu hadi mgongoni,” Shahidi.
Ushahidi wa Jumanne ulitolewa na Watanzania wawili waliokuwa walinzi katika eneo la ubalozi wa Marekani mjini Dar es Salaam, pamoja na mwanamke mmoja ambaye alikuwa msaidizi wa kisiasa katika ubalozi, na mlinzi mmoja wa jeshi la Marine la Marekani.
Valentine Mathew Katunda, mmoja wa walinzi wa Kitanzania alitoa ushahidi kuwa mnamo August 7, 1998, alikuwa katika lindo nje ya ubalozi aliposikia mlio mkubwa kama radi. Akitoa ushahidi kwa Kiswahili kupitia mfasiri, Katunda alisema alijikuta ametupwa sakafuni kutokana na mlipuko huo na kupoteza fahamu. Alipozinduka alijikuta katika kifusi ambapo alibanwa kwa muda wa saa nne nzima.
Naye Justina Mdobilu, mwanasheria wa Tanzania ambaye alikuwa akifanya kazi katika ubalozi kama msaidizi wa maswala ya kisiasa na mfasiri, alieleza mahakama kuwa alikuwa akihudhuria mkutano na naibu balozi alipoona mlipuko nje kupitia dirishani. Alisema dirisha lilivunjikia ndani ya chumba na alichosikia “ilikuwa kishindo kikubwa kuliko vyote nilivyopata kusikia katika maisha yangu, maumivu makali yalipita kifuani kwangu hadi mgongoni.” Mdobilu ambaye alikuwa na mimba ya miezi minane wakati huo alikatika sehemu kadha na kutokwa damu lakini aliweza kutoka katika jengo la ubalozi huo. Mtoto wake alizaliwa bila madhara.
0 comments:
Post a Comment