Watoto wengi walioambukizwa virusi vya HIV hivi sasa wanaishi hadi kubalehe na kuwa vigori,na sababu kubwa ni kuimarika kwa uwezo wa kupata dawa za kurefusha maisha.
Taarifa hizi zimetolewa katika jarida la mwezi huu la shirika la afya duniani WHO. Lakini jarida hilo linasema kuna upungufu mkubwa wa huduma za afya za kukidhi mahitaji maalumu waliyonayo. Jarida hilo linasema kwa mujibu wa takwimu kutoka kusini mwa Afrika zinaonyesha kwamba umri wa kuishi kwa wenye virusi vya ukimwi unabadilika kwani watoto waliopata virusi wakati wa kuzaliwa wakati wa miaka ya 1990, sasa wanaishi hadi umri wa kubalehe au kuwa vigori.
Linasema idadi ya watoto wenye umri mkubwa na vijana inaongezeka na huenda ikawa sawa au kuzidi mzigo wa watoto na vijana wadogo katika siku za usoni hasa wakati huu ambapo matibabu na mipango ya kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ynapatikana kila mahali. Hata hivyo utafiti uliofanyika nchini Zimbabwe umebaini pengo kubwa katika huduma kwa vijana walio balehe na kuwa vigori ambao wameambukizwa virusi vya HIV.
Mmoja wa waandishi wa ripoti hiyo Dr Rashida Ferrand, kutoka London School of Hygiene and Tropical Medicine, anasema vijana hao wana huduma, mahitaji na msaada maalumu .Ameongeza kuwa wanahitaji huduma hiyo maalumu hususani ushauri nasaha ili kuwasaidia kufuatilia tiba la sivyo dawa zitakuwa sugu na kisha kutofanya kazi.



0 comments:
Post a Comment