Rais Kagame awataka viongozi wa Afrika waepuke kutegemea misaada ya kigeni
Rais Paul Kagame wa Rwanda amewataka viongozi wa bara la Afrika waepuke kutegemea misaada ya kigeni na badala yake watumie raslimali zinazopatikana katika nchi zao katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo. Akizungumza kwenye mkutano wa viongozi wa Afrika pambizoni mwa kikao kikuu cha kila mwaka cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani, Rais Kagame amesema kuwa wafadhili wa kigeni ingawa huonyesha kuwa nia yao ni kuzikomboa nchi masikini kutoka kwenye lindi la umasikini, ukweli ni kwamba wao hutumia misaada hiyo kuziainishia nchi hizo sera za kufuata, jambo alilolitaja kuwa ni hujuma dhidi ya uhuru wa kujitawala. Amesema nchi zinazoendelea zinaweza kujisimamia iwapo viongozi wataweka ajenda za maendeleo mbele na kuepuka siasa zisizokuwa na natija.
0 comments:
Post a Comment