Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, P. J. Crowley, aliwaambia waandishi wa habari pembeni ya mikutano ya mwaka kwenye Umoja Mataifa waziri wa mambo ya nje, Hillary Clinton alikutana mapema Jumatatu na makamu rais wa Sudan, Ali Osman Taha.
Bwana Crowley amesema waziri Clinton amethibitisha nia ya dhati ya Marekani katika utekelezaji kamili wa mkataba huo na kurejea kwamba kuna haja ya kuona hatua zinachukuliwa ili kuhakikisha kuwa kura ya maoni inaitishwa kwa wakati muafaka kwa ajili ya wote Sudan kusini na na Abyei ili kuunga mkono mkataba huo wa amani.
Mkataba wa amani wa mwaka 2005 ulimaliza vita virefu vya Sudan vilivyodumu kwa miongo miwili kati ya kaskazini na kusini.
Msemaji Crowley amesema makamu rais Taha alirejea nia ya dhati ya Khartoum kwa mkataba huo, na kukiri kuwa kuna mengi yanahitaji kufanywa kabla ya upigaji kura wa January.
Wanadiplomasia wa magharibi kwenye Umoja Mataifa katika wiki za karibuni walielezea wasi wasi kwamba matayarisho kwa kura hiyo yamekwama. Wana wasi wasi kwamba kuakhirisha upigaji kura, ama kunaweza kuonekana kuwa pengine matokeo yasingekuwa ya uhakika na hii huenda ikairejesha nchi katika ghasia.
Msemaji wa Marekani amesema Washington itampeleka Princeton Lyman, mwanadiplomasia mwandamizi wa Marekani katika eneo hilo wiki ijayo, wakati uwakilishi wa Marekani umeongezeka huko na kuzidisha kazi zake na pande husika. Crowley amesisitiza umuhimu wa Sudan kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa mkataba wa amani na kusema kutakuwa na madhara kama hilo halitafanyika.
0 comments:
Post a Comment