Kenya yatakiwa kuweka wazi msimamo wake kuhusiana na Mahakama ya ICC
Kofi Annan Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa ameitaka serikali ya Kenya kuweka wazi misimamo yake kuhusiana na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, kufuatia safari iliyofanywa hivi karibuni na Rais Omar Hassan al Bashir wa Sudan nchini Kenya. Annan amesema kuwa, Kenya ikiwa ni moja kati ya nchi zilizotia saini makubaliano ya Rome, inalazimika kumtia mbaroni Rais al Bashir ambaye tokea mwezi Machi 2009 anatuhumiwa na mahakama ya ICC kwa kutenda eti jinai za kivita na kibinadamu huko Darfur, magharibi mwa Sudan. Licha ya kutolewa waranti mbili za kutiwa mbaroni Rais al Bashir, lakini kiongozi huyo alielekea nchini Kenya kwa shabaha ya kushiriki kwenye sherehe za kuidhinishwa katiba mpya ya Kenya zilizofanyika siku ya Ijumaa mjini Nairobi. Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, watu walio wengi walishangazwa na hatua ya kushiriki Rais al Bashir wa Sudan kwenye sherehe hizo. Kofi Annan alitoa taarifa hiyo akiwa kama mkuu wa kundi la shakhsia na viongozi mashuhuri wa Kiafrika. Kundi hilo lilipewa jukumu na Umoja wa Afrika la kusaidia mchakato wa kutatua mgogoro wa kisiasa ulioibuka nchini humo baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa rais wa mwaka 2007. Kweye machafuko hayo, watu wasiopungua 1,500 waliuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa.
0 comments:
Post a Comment