Habari kutoka Nairobi mji mkuu wa Kenya zinasema kuwa watu 11 wamefariki dunia huku wengine kadhaa wakipoteza uwezo wao wa kuona baada ya kunywa pombe yenye sumu katika mtaa wa mabanda wa Kibera viungani mwa jiji hilo. Duru za Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta zinasema kuwa watu kadhaa bado wanaendelea kupata matibabu kutokana na tatizo hilo. Duru zaidi zinasema kuwa watu 7 wamefariki dunia leo kwenye hospitali hiyo huku tano wakipatikana manyumbani mwao wakiwa wamefariki dunia usiku wa Jumapili. Polisi ya Kenya imetangaza kuwa tayari imewatia nguvuni watu kadhaa wanaoshukiwa kuwa ndio waliotengeneza pombe hiyo.
Wakati huo huo Mkurugenzi mpya wa Tume ya Kupambana na Ufisadi nchini Kenya KACC amesema leo kuwa atahakikisha wale wote waliohusika na kesi kubwa kubwa za ufisadi wanapandishwa kizimbani. Hata hivyo amekumbusha kuwa vita dhidi ya ufisadi vitachukua muda kabla ya uozo huo kutokomezwa kabisa. Patrick Lumumba alikuwa akizungumza na waandishi wa habari mapema leo kwa mara ya kwanza tangu alipoidhinishwa kuiongoza taasisi hiyo Ijumaa iliyopita.
0 comments:
Post a Comment